Friday, May 5, 2017

Kilimo cha karanga

Karanga ni moja ya jamii ya kunde, ambayo hulimwa lengo kubwa likiwa ni uzalishaji wa mafuta, chakula na malisho kwa ajili ya mifugo. Karanga ni zao maarufu sana duniani katika kilimo cha mzungunguko. Nchini Tanzania uzalishaji wa karanga ni wa chini sana kutokana na kutokuwa na mvua za uhakika, kiwango kidogo cha teknolojia miongoni mwa wakulima, wadudu na magonjwa, pamoja na kutokuwa na mbegu ya uhakika.

Mmea wa karanga ni moja ya mimea mifupi ambayo huota na kuwa na urefu wa sentimita 15-60 kwenda juu. Matunda yake huwa na kati ya mbegu moja mpaka tano, ambapo viriba vyake huwa chini ya ardhi. Mbegu zake huwa na kiasi kikubwa cha mafuta (38% – 50%), protini, kalishamu, potashiamu, fosiforasi, magnesiamu na vitamini. Inasadikiwa kuwa karanga pia zina aina fulani ya viini vinavyotumika kama dawa.

Karanga pia zinaweza kuliwa zikiwa mbichi, zikiwa zimechemshwa au kukaangwa. Zinaweza pia kutengenezwa kama kitafunwa kwa kuchanganywa na sukari au asali. Pia karanga hutumika kwenye supu, mchuzi, au kama kiungo kwenye aina nyingine za vyakula kama vile nyama na wali. Mabaki ya mimea yake ni malisho mazuri sana kwa wanyama.

Hali ya hewa kwa ajili ya kilimo hiki.
Karanga hulimwa kwenye sehemu yenye joto, wastani wa mwinuko wa mita 1500 kutoka usawa wa bahari. Kiwango cha joto kinachohitajika kila siku ni kiasi cha jotoridi 30, na wakati wa ukuaji kinaweza kupungua mpaka jotoridi 15. Hali ya ubaridi huchelewesha karanga kuchanua.

Udongo na kiwango cha maji
Kwa kuwa viriba vya karanga huwa kwenye udongo na ni lazima kuchimbuliwa wakati wa mavuno, huku vikiwa ni vyepesi kuvunjika, ni vizuri kuwa na udongo mkavu, lakini mmea hukua na kustawi vizuri kwenye udongo wa mfinyanzi uliochanganyika na kichanga!

Mvua
Kiasi cha milimita 500-600 cha maji katika msimu wote wa ukuaji wa karanga kinatoa fursa nzuri ya uzalishaji. Hata hivyo karanga ni moja ya mazao yanayostahimili ukame, na linaweza kuvumiliwa ukosefu mkubwa wa maji. Hali inapokuwa hivyo hupunguza kiasi cha mavuno.

Kupanda
Inapendekezwa kupanda kwenye sehemu ambayo udongo una kina na ambao chembechembe zake ni laini. Kuwa makini na uhakikishe kuwa sehemu ya kitalu haina magugu. Kitalu chenye udongo usiokuwa na chembe laini na tambarare inaweza kusababisha upotevu mkubwa wa mimea.

Inapendekezwa kuwa na kiasi cha mimea 200,000 – 250,000 kwenye hekari moja, hasa kwa aina ambayo ni ya muda mfupi. Kwenye nchi nyingi karanga hulimwa kwa kupanda kwenye mistari, ambayo mingi huwa na nafasi ya sentimita 40 x 20 mpaka sentimita 30 x 20.

Baada ya kulima na kusawazisha vizuri, tengeneza matuta yenye mwinuko wa sentimita 80, na sehemu ya juu iwe bapa ili uweze kupanda mistari miwili ya karanga kwenye kila tuta. Ni lazima kuchagua mbegu za kupanda kwa umakini. Ni lazima ziwe safi, zilizojaa vizuri na bila kuwa na mikwaruzo yoyote.

Mbegu zinazokusudiwa kupandwa ni lazima ziachwe kwenye viriba vyake na kumenywa siku chache kabla ya kupanda. Kina cha upandaji wa karanga ni sawa na mahindi ambapo huwa kati ya sentimita 5-8.

Kuna aina mbili za karanga:

  • Aina ya mafungu
  • Aina inayotawanyika

Aina zinazolimwa Tanzania ni pamoja na Johari, Pendo, Nyota, Sawia, Mamboko.

Matunzo
Ili kuwa na mavuno ya hali ya juu, ni lazima magugu yadhibitiwe kabisa. Karanga ni dhaifu sana katika kukabiliana na magugu hasa katika kipindi cha mwanzo cha ukuaji. Ni lazima palizi ifanyike mapema wakati huo miche ikiwa inachomoza kwenye udongo. Miche ikashachomoza palizi ifanyike kwa mikono ili kuepuka usumbufu kwa karanga changa au kuharibu maua.

Palizi ya kawaida inaweza kufanyika mpaka kwenye kipindi cha wiki 6 na palizi ya mikono ifanyike baada ya hapo.

Virutubisho pekee vinavyohitajika kwenye shamba la karanga ni kalishamu. Kalishamu hunyonywa moja kwa moja na viriba vya karanga endapo udongo una unyevu unyevu. Kama kutakuwepo upungufu wa kalishamu, viriba vya karanga vitakuwa vitupu bila kuwa na karanga. Mimea inayohitaji Naitrojeni inaweza kupatikana kwa kushirikisha mimea mingine kama vile kunde, badala ya kuweka mbolea ya Naitrojeni kwenye udongo.

Mavuno
Karanga zinazokomaa kwa muda mfupi zinaweza kuvunwa kati ya siku 85-100 tangu kupandwa, na zinazochukua muda mrefu zinaweza kuvunwa katika kipindi cha siku 110-130 tangu kupandwa. Ng’oa mashina machache kuona kama karanga zimeshakomaa. Karanga zilizokomaa ni lazima ziwe na rangi ya kahawia kwa nje, ngumu na zilizokauka.

Kwa kawaida karanga zilizokomaa ndani ya kiriba huwa na rangi ya kahawia, na hutoa sauti inapotikiswa. Magonjwa yanaposhambilia majani ya karanga yanaweza kusababisha karanga kuvunwa kabla hazijakomaa sawa sawa. Ni lazima karanga zichimbwe kwa umakini ili kuepuka karanga kupasuka na kubakia ardhini.

Anika kwa siku 2-3, kisha zikwanyue na uanike tena kwenye jamvi kwa siku 7-10 ili kuondoa unyevu kufikia asilimia kumi.

Ubambuaji wa karanga ufanyike kwa mikono au kwa mashine maalum. Karanga zilizopondeka, chafu au kuharibika zitengwe kwani zitapunguza ubora wa karanga na kupunguza bei ya kuuzia.

Endapo karanga hazikuhifadhiwa vizuri zinaweza kushika unyevu unyevu ambao husababisha sumu inayojulikana kama aflatoxin ambayo ni hatari sana kwa afya ya binadamu hasa ini. Karanga ambazo zitatumika kwa ajili ya kupanda (mbegu) msimu unaofuata zisibambuliwe kutoka kwenye viriba.

Na kufikia hapo hatuna la ziada tukutane siku nyingine ambapo tutazungimza kilimo cha kunde.

No comments:

Post a Comment