Mfumo wa kilimo cha mseto hujumuisha yafuatayo:
- Ukuzaji wa mimea na miti ya aina fulani kwa pamoja kwenye shamba. Mfumo huu waweza kuandaliwa kwa zamu au hata kujumuishwa kwa pamoja bila kuzingatia msimu.
- Mifugo na mimea ya chakula hujumuishwa kama sehemu ya mfumo huo.
Ni muhimu kufahamu kwamba hakuna njia moja ya kuimarisha na kufanikisha kilimo, bali mbinu za kila aina zapaswa kutekelezwa. Mbinu hizi zaweza kujumuisha jamii nzima katika kupanda miti ya kienyeji, miti mingine yenye manufaa, mbinu za kutunza udongo na njia nyinginezo za kuimarisha kilimo cha mseto. Kilimo cha mseto hunufaisha sehemu kame, zile zisizotumika kwa kikamilifu au hata zile za tindikali au udongo wa chumvi nyingi.
Faida za mfumo wa kilimo cha mseto
Iwapo shamba ni dogo au ni eneo lisilo na rutuba au hata mahali palipoathiriwa na mmonyoko wa udongo, mfumo wa kilimo cha mseto hufaa sana. Miti inayo umuhimu kwenye mazingira na uchumi. Yafuatayo ni manufaa ya kilimo cha mseto:
Udongo
- Kuzuia mmomonyoko wa udongo.
- Kuimarisha rutuba ya udongo.
- Kuimarisha umbo na kutunza unyevunyevu wa udongo.
Nguzo ya kawi
- Mfumo huu hutoa kuni kwa matumizi ya nyumbani.
- Kila aina ya mti hutoa kiwango fulani cha kuni au makaa.
Ujenzi na useremala
- Viungo vya ujenzi kama mbao na fito.
- Katika ujenzi wa uwa na zizi ili kuzuia mahasimu kuvamia mifugo.
- Miti ni nguzo kuu katika kuzuia upepo mkali au hata kutoa kivuli.
Uhai-anuai
- Mfumo huu huendeleza mandhari ya kimaumbile.
- Mfumo huu huendeleza miti na mimea ya kiasili. Hali ya Kiuchumi
- Kama njia ya kutoa nafasi zaidi za kazi.
- Mapato kutokana na mauzo ya bidhaa za miti.
- Njia bora ya uwekezaji kama kukuza matunda na baadhi ya mazao mengineyo.
Kupanda miti bila kuzingatia utaratibu
Miti yaweza kukuzwa pamoja na mazao mengine pasipo kuzingatia utaratibu fulani. Waweza kuendeleza miti iliyoko au kukuza mingine katika eneo hilo. Miti hii yaweza kuwa ya matumizi ya nyumbani au kwa shughuli za kiuchumi kama vile chakula, kuni, fito, mbao au chakula cha cha mifugo. Miti husaidia sana katika kuimarisha umbo na rutuba ya udongo. Utaratibu huu hutegemea aina ya jamii ya miti na aina ya mimea inayokuzwa, katika mfumo huu miti hupandwa kwa upana wa kuanzia mita nane hadi 10 au zaidi.
Faida:
- Kupanda miti kwenye eneo la mimea husaidia sana katika kuimarisha rutuba, kuweka kivuli na kutoa viungo vya mboji.
- Miti ni ngome na mahali pa wadudu na wanyama wenye manufaa wanaoshambulia wadudu waharibifu.
- Mazao ya miti yaweza kutumiwa katika shughuli za kuinua uchumi au kwa matumizi ya nyumbani.
Upungufu
- Miti yaweza kuvutia wadudu na wanyama waharibifu.
- Miti yaweza kusababisha ushindani wa kupata maji na madini. Ni bora iwapo kina cha mizizi ya miti ni kikubwa kuliko kile cha mimea inayoambatanishwa
Kuzingatia safu
Mfumo huu huzingatia safu. Safu za miti hupandwa kwa kuambatanisha na safu za mimea mingine kwa kuzingatia utaratibu maalum. Lengo kuu la mfumo huu ni kuimarisha rutuba na idadi ya mazao. Mfumo huu hufaa sana katika sehemu za majira ya baridi au zile zenye hali ya juu ya unyevu. Mfumo huu huweza kusaidia sana katika kuimarisha umbo la udongo na kuongeza rutuba. Mfumo huu kadhalika huhitaji uangalifu. Aina ya miti inayotumiwa isiwe ile ya kufanya kivuli kupita kiasi. Mimea yapaswa kupata kiwango kizuri cha jua. Itakuwa bora iwapo mkulima atapogoa miti ili kuondoa matawi ya ziada. Miti iliyotumiwa yapaswa pia kuendelea vyema licha ya kupogolewa. Ufuatao ni utaratibu wa mfumo huu:
Utaratibu wa mfumo wa kuzingatia safu
- Miti hupandwa kwa safu ikiambatanishwa na safu ya mimea mingine.
- Miti hupogolewa au kukatwa iwapo mimea itaathiriwa.
- Matawi yaliyopogolewa hubakia shambani ili kutengeneza mboji na kuimarisha rutuba. Vijiti au sehemu zilizokomaa zaweza kuchukuliwa kwa matumizi ya kuni.
- Licha ya kukatwa au kupogolewa, miti hujitokeza upya.
- Utaratibu kurejelea.
Faida:
- Kiwango cha juu katika kuimarisha rutuba na umbo la udongo hufikiwa.
- Matumizi muafaka ya shamba na kwa kikamilifu.
- Miti iliyotumiwa yaweza kuwa na faida ya kinyumbani au ya kiuchumi.
Upungufu:
- Mfumo huu huchukua miaka mingi kabla ya kuafikiwa, hivyo basi itachukua muda kabla ya kuona faida.
- Wakulima waweza kukosa pesa za kununua miche ya miti inayostahili.
- Mfumo huu huhitaji kazi nyingi sana. Iwapo miti haitakatwa au kupogolewa kwa wakati, mimea huathiriwa.
- Mfumo huu husababisha ushindani usiofaa baina ya miti na mimea. Ni bora kupanda miti iliyo na mizizi ya kina kirefu kuliko ile ya mimea iliyoambatanishwa.
Kilimo mseto: Uhakika wa chakula, utunzaji wa mazingira
No comments:
Post a Comment