Wednesday, June 21, 2017

KILIMO CHA ZAO LA VANILLA - PART 2

Uzalishaji-wa-zao-la-vanilla

 Katika kipindi kilichopita tuliona mahitaji ya zao la vanilla na jinsi linavyolimwa, sasa leo napenda kukukaribisha ndugu yangu mkulima katika sehemu hii ya pili ambapo tutaona: magonjwa na wadudu waharibifu wa zao la vanilla likiwa shambani pamoja na kuvuna, kukausha na soko lake. Karibu...


MAGONJWA, WADUDU NA WANYAMA WAHARIBIFU

Mmea wa vanilla kwa kawaida haushambuliwi mara kwa mara na magonjwa au wadudu waharibifu kama shamba limetunzwa vizuri. Mashambulizi ya magonjwa na wadudu waharibifu ni dalili ya utunzaji duni wa shamba. 

Ili kuepuka hali hiyo, ni muhimu kukagua shamba kila wakati kubaini na kurekebisha yafuatayo:
  • Nafasi kati ya mmea na mmea ni ya kutosha kuruhusu mzunguko wa hewa safi na hivyo kupunguza hali inayoruhusu vimelea vya magonjwa kuishi na kuzaliana.
  • Kivuli kisiwe kizito ili kuepuka giza linalowavutia wadudu waharibifu na kuruhusu vimelea vya magonjwa.
  • Kivuli chepesi husababisha kuungua kwa majani na kufanya mmea kutokua vizuri
  • Afya ya mmea ikaguliwe kwa makini.
Kulisha marando kila mara kunaongeza uwezo wa mizizi kuchukua chakula ardhini hivyo mmea hukua vizuri. Mmea wenye afya nzuri haushambuliwi na magonjwa pia hustamilii mashambulizi ya wadudu waharibifu.

Magonjwa

(i) Kuoza kwa Mizizi (Root rot)

Ugonjwa huu husababishwa na kuvu inayoitwa Fusarium batatis Woollenw.var. vanillae Tucker.

Dalili
  • Mmea kunyauka na majani kuningíinia.
  • Majani kubadilika rangi na kuanza kuwa ya manjano na hatimaye kukauka.
  • Mmea kunyauka sehemu ya chini iliyo kati ya shina na mizizi.


Kudhibiti
  • Ondoa maji yaliyotuama.
  • Epuka kujeruhi mizizi.
  • Tumia dawa za ukungu kama Bordeaux mixture 5%.

(ii) Chule ya Majani, Matunda (Anthracnose)

Ugonjwa huu husababishwa na aina ya kuvu inayojulikana kama Calospora vanillae Massee.

Dalili
  • Mapodo na majani kuwa na madoa ya rangi ya kahawia.
  • Majani na ncha ya juu ya shina hunyauka.
  • Mizizi na mapodo na hunyauka
  • Mapodo hudondoka


Kudhibiti
  • Kuzuia maji yasituame ardhini
  • Kutengeneza kivuli chepesi,
  • Kupunguza matawi
  • Kuzingatia nafasi kati ya mmea na mmea ili kuruhusu hewa safi kupita vizuri.
  • Kunyunyizia dawa aina ya Bordeaux mixture (1%) au Captafol 0.1% kabla ya mimea kuchanua.

(iii)Ubwiri Vinyoya (Downy mildew)

Husababishwa na kuvu aina ya Phytophthora jatrophae Jens ambao hushambulia mti wa Jatropha unaotumika kama muega. Pia hushambulia mapodo yakiwa shambani na baada ya kuvunwa.

Dalili: Mapodo ya vanilla na majani ya jatropha huwa ukungu mweupe.

Kudhibiti
  • Kufuata kanuni bora za utunzaji wa shamba.
  • Kutumia dawa za ukungu kama Nitrophenol 0.518 

Wadudu, Ndege na Wanyama Waharibifu

(i) Wadudu

Wadudu wanaoweza kushambulia vanilla ni pamoja na katapila na jongoo.

  • Katapila: Hukata ncha ya mmea inayokua


Kudhibiti: Kagua shamba mara kwa mara ili kutambua kuwepo kwa wadudu hao na kuwaua.

  • Jongoo: Hukwangua shina na kuacha michubuko


Kudhibiti: Kagua shamba mara kwa mara na kuwaua.

(ii) NdegeKuku

Huharibu mmea kwa kuparura juu ya ardhi na kusababisha kujeruhi na kukata mizizi. Uharibifu huu husababisha mmea kuwa katika mazingira rahisi ya kushambuliwa na vimelea kama Fusarium batatis ambao huozesha mizizi ya mmea.

Kudhibiti: Zuia kuku wasiingie shambani.

(iii) Konokono

Husababisha uharibifu zaidi kipindi cha mvua. Wanapotambaa kwenye mmea huacha utando, hasa katika sehemu inayochipua na kusababisha mmea kudumaa.

Kudhibiti
  • Kagua shamba mara kwa mara na kuwaondoa.
  • Weka mchanganyiko wa mbolea ya samadi na majivu kuzunguka shina la mmea ili kuzuia wasiweze kupanda juu ya mimea.

UVUNAJI

Mapodo ya vanilla hukomaa na kuwa tayari kuvunwa baada ya miezi sita hadi tisa tangu maua kuchavushwa.

Hatua za Kukomaa kwa Vanilla

Ukomaaji wa podo (harage la Vanilla) la vanilla hupitia hatua tano zifuatazo:
  1. Podo hurefuka na kuwa na rangi ya kijani iliyokolea.
  2. Ncha ya podo hubadilika na kuwa njano.
  3. Rangi ya njano husambaa taratibu katika podo.
  4. Ncha ya podo hubadilika rangi na kuwa ya kahawia
  5. Podo hupasuka kuanzia chini.

Jinsi ya kuvuna

Uvunaji wa zao la vanilla huzingatia hatua za ukomaaji wa podo na njia ya ukaushaji itakayotumika. Mapodo huvunwa kwa kukata kikonyo kutumia kisu kidogo.
  • Katika hatua ya kwanza ya ukomaaji, mapodo hayana vanillin ya kutosha hivyo yasivunwe katika hatua hiyo.
  • Mapodo yanaweza kuvunwa yakiwa katika hatua ya pili na ya tatu endapo yatakaushwa kwa njia ya Bourbon.
  • Mapodo yanayokaushwa kwa njia ya kukata na kukausha haraka huvunwa yakiwa katika hatua ya pili, ya tatu na ya nne. Mapodo yasiachwe hadi kufikia hatua ya tano ya ukomaaji kwani ubora wake hupungua.
  • Uvunaji ufanyike kila baada ya siku moja hadi mbili ili kuepuka kupasuka kwa mapodo.
  • Uvunaji huendelea kwa muda wa miezi miwili mfululizo au zaidi kulingana na ukomaaji wa mapodo.
  • Marando yaliyosisimuliwa na kutoa mapodo yakatwe na kuondolewa shambani baada ya kuvunwa.

Vanilla-iliyovunwa


Mavuno

Mavuno ya zao la vanilla hutofautina kulingana na umri wa mmea na utunzaji wa shamba. Mavuno ya kwanza huanza kati ya miaka miwili na nusu hadi mitatu kwa wastani wa kilo moja sawa na mapodo 50 hadi 60. Mmea unapofikia umri wa miaka minne hadi nane, mavuno huongezeka kufikia kilo tatu hadi tano kwa mmea. Hata hivyo mavuno huweza kupungua mmea unapofikia miaka 15 na kuendelea. Hekta moja ya shamba la vanilla lililotunzwa vizuri hutoa mavuno tani tatu hadi tano za mapodo mabichi sawa na wastani wa kilo 500 hadi 800 za mapodo yaliyokaushwa kwa mwaka.


UKAUSHAJI NA UHIFADHI

Mapodo ya vanilla hukaushwa kwa njia mbalimbali kulingana na utaalamu unaotumika, vifaa vilivyopo na matakwa ya mnunuzi. Ili kupata ubora unaotakiwa, mapodo yakaushwe mara baada ya kuvunwa. Njia za ukaushaji zinazotumika zaidi ni Bourbon na Mexico. Njia hizi huhitaji uangalifu na utaalamu wa kutosha ili kupata madaraja mbalimbali, ladha, na harufu inayohitajika. Njia zote mbili hupitia katika hatua kuu nne za ukaushaji. Hapa nchini, njia ya ukaushaji inayotumika kwa sasa ni Bourbon.



Ukaushaji kwa Njia ya Bourbon

Njia hii ya ukaushaji huhusisha hatua zifuatazo:

Kuchovya Mapodo kwenye Maji moto (Blanching).

Hatua hii huyazuia mapodo yasiendelee kukomaa na kuanza kutoa ladha.
  • Mapodo mabichi hupangwa kulingana na ukubwa na hatua za ukomaaji.
  • Mapodo hayo hupangwa katika mafungu yasiyozidi uzito wa kilo 30 ili kurahisisha uchovyaji.
  • Mapodo huwekwa na kufungwa katika mifuko ya vitambaa maalumu vinavyoruhusu joto la maji kupenyeza kwa urahisi.
  • Mapodo yaliyovunwa katika hatua ya pili, tatu, na nne ya ukomaaji, yatumbukizwe katika maji yenye joto la nyuzi 60 hadi 65 za Sentigredi kwa muda wa dakika tatu hadi tatu na nusu.
  • Mapodo yaliyovunwa katika hatua ya tano ya ukomaaji, yatumbukizwe kwenye maji ya moto kwa muda usiozidi dakika moja.
  • Mapodo yaliyochovywa kwenye maji ya moto vizuri, huwa na rangi ya kijani iliyokolea hadi kahawia.

Kuhifadhi Joto (sweating)

Lengo la hatua hii ni kuongeza joto katika mapodo ili kuruhusu vimengíenya (enzymes) kufanya kazi ya kutoa kemikali ya vanillin ambayo huongeza ladha na harufu inayohitajika.
  • Mapodo yaliyochovywa maji moto hutolewa maji na kufungashwa katika vitambaa vyeupe na mablanketi yanayoweza kuhifadhi joto.
  • Mapodo huwekwa kwa muda wa siku moja hadi mbili (saa 24 hadi 48) katika makasha maalumu yanayohifadhi joto.
  • Mapodo hutolewa kwenye makasha baada ya siku moja au mbili na kutandazwa ili kuondoa yasiyo na rangi ya kahawia.
  • Katika hatua hii, mapodo huwa na rangi ya kahawia iliyokolea.

Kukausha

Katika hatua hii, mapodo huanikwa asubuhi au jioni wakati jua sio kali.
  • Mapodo yaliyofungashwa kwenye vitambaa vyeupe na mablanketi hutandazwa juu ya vichanja na kuanikwa kwa muda wa saa moja au mbili.
  • Baada ya saa moja au mbili, mapodo hufungashwa tena kwenye mablanketi na kurudishwa ndani. Kazi hii huendelea kwa muda usiopungua wiki tatu.
  • Baada ya wiki tatu, mapodo hutandazwa ndani, juu ya vichanja vinavyoruhusu hewa ya kutosha.
  • Ukaushaji wa ndani huchukua muda wa miezi mawili au mitatu.
  • Ukaguzi ufanywe mara kwa mara ili kuondoa mapodo yenye hitilafu na kutenga yaliyowahi kukauka.

Vanilla-iliyokaushwa


Kuhifadhi Ladha

Hii ni hatua ya mwisho katika mtiririko mzima wa ukaushaji. Katika hatua hii, mapodo huwekwa katika makasha maalumu kwa muda wa miezi mitatu hadi mitano ili kuongeza ladha ya vanilla.


Kufungasha

Vanilla iliyokwisha kaushwa vizuri hufungashwa kulingana na madaraja. Uzito wa kila kifungu na aina ya ufungashaji hutegemea mahitaji ya soko.

No comments:

Post a Comment