Saturday, June 10, 2017

MBINU ZA MSINGI ZA KUTHIBITI MAGONJWA NA WADUDU KATIKA KILIMO CHA MBOGA

Habari ndugu mkulima mwenzangu, ni matumaini yangu unaendelea vyema katika safari ya kusaka mafanikio. Kitu cha muhimu sana unachopaswa kufahamu ni kwamba Mafanikiokatika jambo lolote hutegemea sana na kiwango cha MAARIFA kwenye jambo husika. Hata mafanikio kwenye kilimo yanategemea sana na maarifa uliyonayo kuhusu kilimo husika. Hivyo basi usiache kujifunza mara kwa mara. Ni heshima kwangu kupata fursa hii ya kua mwalimu na kocha wako wa masuala ya kilimo biashara kupitia blog hii ya Kilimobiashara (www.kilimobiashara.net). Leo tunakwenda kujifunza kuhusu MBINU ZA MSINGI ZA KUTHIBITI MAGONJWA NA WADUDU KATIKA KILIMO CHA MBOGA.  Japo mafunzo yameongelea zaidi  kudhibiti magonjwa na wadudu kwenye mboga, lakini mbinu nyingi hapa zinatumika pia  kwenye mazao mengine, nafaka, mikunde, matunda n.k Karibu sana.
Madhara ya magonjwa na wadudu
a)  Hupunguza   kiasi   cha   mavuno   na  hata   kuua   mimea kabisa.
b)  Hupunguza ubora wa mboga.
c)  Huongeza   gharama   za   uzalishaji,   hasa   madawa   ya viwandani yanapotumiwa.
d)  Huongeza uharibifu wa mboga baada ya kuvuna.
Namna  ya  kutambua   magonjwa   na  wadudu   washambuliao mboga:
Lazima utambue aina ya ugonjwa au mdudu ili utumie kinga ianayostahili.   Hii  siyo  kazi  rahisi.   Zifuatazo   ni  baadhi   ya  njia ambazo unaweza kutumia:
a)   Kutumia uzoefu wako, hasa baada ya kuwa na wataalam wa wadudu na magonjwa ya mimiea kwa muda mrefu.
b)   Kutumia mabwana shamba.
c)   Kutumia wataalam wa magonjwa na wadudu wa mboga.
d)   kuchunguza sehemu ya mmea uliyougua kwenye maabara.
Kanuni za kukinga mboga dhidi ya magonjwa na wadudu
Kabla   hujaamua   kutumia   madawa   ya   kienyeji   au   viwandani, hakikisha unafanya mambo yafuatayo hatika bustani yako:
Chagua udongo usiokuwa na magonjwa ya mboga unayotaka kuzalisha.
Tumia  mbegu  bora,  kwani  baadhi  ya  magonjwa  hutokana  na mbegu.
Hakikisha kuwa vitalu, bustani na sehemu ya kuhifadhi mboga ni safi.  Uchafu  na  magugu  huvutia  magonjwa  na  wadudu waharibifu.
Toa  majani  au  mimea  iliyokwisha  ugua,  na  ichome  moto  au ifukie.
Panda  mazao  muda  unaotakiwa  ili  kukwepa  baadhi  ya magonjwa ya msimu.
Epuka  kupanda  mboga  ya  jamii  moja  katika  eneo  moja  kwa misimu mingi mfululizo. Mfano Nyanya, Pilipili Hoho, Ngogwe na Viazi mviringo ni jamii moja ya Solanaceae. Mazao haya hayapaswi kupandwa eneo  moja  kwa misimu mfululizo.
Changanya mazao au mimea ambayo inafukuza magonjwa na wadudu kama vile mimea inukayo.
Epuka kuchanganya mboga na baadhi ya mazao yanayovutia magonjwa au wadudu katika bustani yako. Mfano mazao kama mipapai  na  bamia  huvutia  nzi  wadogo  weupe  wanaoeneza ugonjwa wa “ukoma wa nyanya”.
Mwisho,  tumia  madawa  ya  asili  na  viwandani  ili  kupunguza kuenea kwa magonjwa na wadudu. 
Kanuni   za   kukinga   magonjwa   na   wadudu   kwa   kutumia madawa
Unalazimika kukinga mboga dhidi ya magonjwa na wadudu kwa kutumia   madawa   ya   asili   na viwandani   pale   mbinu   nyingine ambazo zimetajwa hapo nyuma zinaposhindwa kuleta mafanikio.
 Zifuatazo ni baadhi tu ya kanuni ya kutumia madawa ya asili na viwandani:

  •   Kwa usalama wa mlaji, unashauriwa kupiga madawa hasa ya viwandani siku 14 kabla ya kuvuna mboga. Pia epuka kupiga madawa mara kwa mara.
  • Epuka  Kupiga  dawa  ya  aina  moja  mara  kwa  mara  dhidi  ya ugonjwa au mdudu wa aina moja   kwani   kufanya   hivyo huwafanya wadudu kujenga sugu dhidi ya dawa hiyo.
  • Epuka  kupiga  dawa  wakati  wa upepo  mkali au jua kali sana kwani kiasi kikubwa cha dawa kinaweza kupotea hewani. Pia usipige dawa wakati wa mvua (mara tu kabla ya mvua) kwani maji ya mvua yataosha na kupunguza nguvu ya dawa.
  • Piga  dawa  wakati  wa  asubuhi  hasa  kukinga  magonjwa  ya ukungu yapendayo unyevunyevu. Kwa kuzuia wadudu, ni vizuri kupiga  dawa  wakati  wa  jioni.  Wakati  wa  jioni  dawa  huua wadudu zaidi kwani hukaa muda mrefu juu ya majani kabla ya nguvu yake kuharibiwa na jua.
  •  Weka  kiwango   cha  dawa  kama  ilivyo  elekezwa   na watengenezaji  au watalaam. Kiasi kidogo cha dawa katika maji hufanya viini vya magonjwa na wadudu kuwa sugu.
  • Zingatia kuwa kiasi cha sumu ndani ya kasha au kopo la dawa hutofautiana kati ya kampuni na kampuni iliyotengeneza. Ikiwezekana tafuta ushauri kwa muuza madawa au wataalam waliokaribu nawe.
  • Piga dawa ya kutosha sehemu zote za mmea kwani baadhi ya wadudu  au magonjwa  hukaa na kushambulia  sehemu  ya chini ya majani.
  • Andaa  vizuri  bomba  la kupigia  dawa  kabla  ya kuchanaganya dawa na maji ili dawa iweze kutoka vizuri.
  • Madawa   hutofautiana   sana   nguvu   za  kuua   wadudu,   hivyo changua madawa yanayofaa kufuatana na ugonjwa na wadudu.
Baadhi ya madawa ya asili
Madawa ya asili ni mengi ila bado hayajafanyiwa utafiti wa kutosha. Baadhi  ya  mimiea  inayotoa  madawa  ya  asili  ambayo yameshajaribiwa  Tanzania  ni muarobaini  (mbegu na majani), kitunguu  swaumu,  manung’anung’a,  tumbaku,  pilipili  kali,  pareto, n.k. Muarobaini ni miongoni mwa mimea michahce ambayo mpaka sasa imefanyiwa utafiti wa kiina. Mfano, kuchanganya nusu kilo ya mbegu  za  muarobaini   zilizotwangwa   katika  lita  ishirini  za  maji husaidia kuua wadudu mbalimbali wakiwemo funza wanaotoboa matunda ya nyanya.
Uzuri na Hasara za Madawa ya Asili
Madawa  ya asili ni bora zaidi kuliko madawa ya viwandani  kwani sumu yake ni kidogo na hupungua  haraka baada ya kupiga dawa. Hivyo ni salama zaidi kwa mpigaji dawa na mlaji mboga. Hivyo kupendekezwa katika kilimo hai na hifadhi ya mazingira
Kasoro kubwa katika kutumia madawa ya asili ni kama zifuatayo:
  • Hayajafanyiwa   utafiti   wa  kutosha ukilinganisha   na yale   ya viwandani. Mfano, nitumie dawa ipi inayofaa kwa mdudu yupi?.
  • Yanakinga zaidi  mboga  dhidi ya  wadudu   waharibifu   kuliko magonjwa.
  • Uwiano wa kuchanganya dawa na maji bado haujulikani vizuri. Mfano, niweke kiasi gani cha dawa katika kiasi gani cha maji?
  • Kwa kuwa nguvu   yake ni kidogo, hayatafaa kuzuia mashambulizi makubwa ya magonjwa au wadudu.
Uzuri na kasoro za madawa ya viwandani.
Madawa  ya  viwandani  yana  sumu  nyingi  zaidi  na  hivyo  huzuia haraka   zaidi   mashambulio   ya   magonjwa   na   wadudu.   Hivyo, hutumika  sana  katika  kilimo  cha  mboga  na  mazao  mbali  mbali kuliko  madawa  ya kienyeji.  Tatizo  la haya madawa  ni kwamba  ni hatari  kwa  mkulima,  mlaji  wa mboga,  mazingira  na pia gharama zake ni kubwa

No comments:

Post a Comment