Sunday, September 24, 2017

JINSI YA KULIMA PILIPILI MTAMA (BLACK PEPPER)

Katika kuabarishana fursa lukuki zilizoko kwenye maeneo tofauti tofauti ndani ya inchi yetu leo Muungwana Blog tunakuletea fursa ya kilimo katika zao la pilipili aina yab mtama (Pilipili Mtama) kwa lugha ya kingereza inajulikana kama black pepper.

Katika kuangalia fursa hii tutagusia maeneo yafuatayo:


  • Utangulizi,
  • Upandaji,
  • Uvunaji,
  • Masoko,
  • Hitimisho

UTANGULIZI
Pilipili mtama ni zao ambalo kitaalamu linajulikana kama Piper nigram ambalo asili yake ni upande wa mashariki ya mbali.Zao hili kwa lugha ya kingereza linajulikana kama BLACK PEPPER.Yapo baadhi ya mikoa au maeneo watu wamekuwa wakijishughulisha na kilimo hichi lakini makala nyingi zinaonesha kuwa kilimo hichi kwa hapa Tanzania hulimwa kwa wingi Zanzibar na mkoani Tanga.

Aina hii ya pilipili imekuwa ikitumiwa zaidi kama kiungo kwenye vyakula mbalimbali hapa kwetu Tanzania na kwa inchi za wenzetu na kwa baadhi ya sehemu kubwa za mashariki ya mbali ni moja katika baadhi ya viungo vinavyofanya vyema sana kibiashara.

Labda kutokana na kuchangia katika mmengenyo wa chakula inapotumiwa kama kiungo katika chakula ndio sababu inafanya kiungo hichi kupendwa zaidi.

UPANDAJI
Ili kupanda zao hili ni lazima kuzingatia mambo kadhaa ili kuweza kupata mazao yakutosha.Mambo hayo ni kama:


  • Hali ya hewa,
  • Udongo,
  • Mbegu bora,
  • Mbolea,
  • Nafasi katika zoezi la upandaji.
  • Miti ya kusimika.
  • Mambo tajwa hapo juu ni lazma yazingatiwe ili kuhakikisha unapata mazao bora yanayokidhi mategemeo yako kibiashara na yanayoendana na malengo yako.


Hali ya hewa ya wastani wa nyuzi 24-26 ndio nyuzi joto zilizoshauriwa katika makala mbalimbali pia ikiwa na wastani wa mvua za mililita 1500 mpaka 2000 kwa mwaka.Pamoja na hali ya hewa inayokidhi ni lazma swala la udongo lihakikishwe limechekiwa .Udongo wenye rutuba na unaopitisha maji.

Tunashauri pia kuwa na utaratibu wa kupima udongo kwa wataalamu wanaotambuliwa ili kuweza kufahamu pH ya udongo wako ili kulinganisha na pH inayotakiwa kwaajili ya kilimo cha zao hili ambayo makala nyingi zinasema ni pH=6.5 .Pia zoezi hili litakusaidia kufahamu baadhi ya wadudu waharibifu wanaoweza kuwepo kwenye udongo ili kuja na njia madhubuti za kukinga kabla ya kuanza kilimo au wakati wa zoezi la ulimaji na hii itasaidia kupata mazao bora.Zoezi hili kama litakuwa ni la umwagiliaji unaweza pia kijiridhisha pia kwa kupima maji yako pia.

Katika kuchagua aina ya mbegu ni vyema kuwashirikisha maafisa/wataalamu wakilimo ili kuepusha kupata hasara kwa kutokuwa na uhakika lakini tofauti ya mbegu hizi huwa hata kwenye umbile la matunda.Lakini uchaguzi wa mbegu huzingatia mambo yafuatayo:


  • Urefu wa pingili na ukubwa wa majani,
  • Ufupi wa pingili na udogo wa majani.

Mbolea nalo ni swala muhimu hakikisha kupima udongo wako ili kujua aina ya mbolea itakayotumika pamoja na wingi/kiwango cha mbolea.Katika ulimwengu wa sasa nyakati za kubahatisha zimepita ni vyema kuzingatia taratibu za kilimo bora ili kupata mazao bora.

Katika zoezi la upandaji ni vyema kuhakikisha nafasi kati ya mche na mche inaanzia mita mbili mpaka tatu. Ni vyema pia kuandaa miti ya kusimika ili zao husika liweze kukua kwa kujizungusha kwenye miti husika.Ni vyema kuhakikisha zoezi la kupunguza majani linafanyika kila msimu ili kupunguza giza katika mimea.

Makala mbalimbali zinaeleza kuwa miche ikishafikia umri wa miezi 18 inapaswa kupunguzwa kwa kukatwa sehemu za juu za miche ili kusaidia matawi mengine yachipue kwa chini.Kiutaalamu wanashauri miche iwe na urefu wa mita tatu mpaka tatu na nusu.

UVUNAJI
Uhalisia wa kilimo hichi unaonesha maua ya kwanza hutokea baada ya miezi 24 yaani baada ya miaka miwili wastani tokea kupandwa.Na matunda yake hukomaa miezi tisa hadi kumi.Zoezi la uvunaji linaweza chukua mzunguko mitano mpaka sita.

Utafiti Muungwana Blog ulioufanya unaonesha endapo zao hili baada ya kuchumwa na kuweka kwenye chombo kisichopitisha hewa basi inaweza kukaa muda mrefu sana bila kuharibika.

MASOKO
Soko la fursa ya zao hili imezidi kukua kwa kasi sana na ndio maana inchi zinazozalisha kwa wingi zao hili kama Vietnam, Indonesia na India na kuchangia katika vyanzo vya ajira na pia katika kuchangia katika biashara mbalimbali zinazochangia katka uchumi.Fursa ya masoko kwa zao hili bado ni kubwa sana kulinganisha na kiwango cha uzalishaji kilichoko kwa sasa hapa inchini.Masoko ya zao hili yapo kwa wingi hapa inchini kutokana na matumizi ya zao hili kama kiungo na pia soko lake lipo kubwa sana ichi za jirani na Tanzania na mashariki ya mbali.

HITIMISHO
Fursa hii bado ni fursa pana na nafasi kubwa kwa wale wote wanaopenda kilimo cha zao hili. Japokuwa kidunia bado tunaona wazalishaji wakubwa kwa  sasa ni  Brazil, India, Indonesia, Malyasia, na Sri Lanka ambao hizi ndizo zinazotambulika na jumuiya ya kimataifa ya IPC (International Pepper Community).

Inchi yetu bado ipo katika wazalishaji wadogo wa pilipili mtama kidunia.Bado uzalishaji mkubwa unaitajika kukidhi soko la ndani na kulenga soko la nje kwa lengo ya kutanua biashara yako na kufanya biashara kimataifa.

No comments:

Post a Comment