Monday, October 23, 2017

Kilimo Bora cha Nyanya; Maandalizi Ya Mbegu, Shamba Na Upandaji Wa Miche

Habari ndugu msomaji wa wetu wa makala za kilimo, Natumaini tunaendelea vizuri na mapambano ya kila siku. Leo tutaanza kujifunza kilimo cha bora cha nyanya, na tutaanza kufahamu vitu vya msingi kwanza, na natumaini ukimaliza mfululizo wa makala hizi utakua mkulima hodari wa nyanya. Kila kitu lazima kiwe na msingi imara, karibu tujifunze wote:

Utangulizi:
• Nyanya ni zao la mboga ambalo hulimwa sehemu nyingi duniani kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na pia kama zao la biashara. Inahisiwa kuwa asili ya nyanya ni nchi ya Peru/Equador huko Amerika ya Kusini. Mmea huu ulianza kuzalishwa kama zao katika nchi ya Mexico na baadaye kusambaa katika nchi nyingine za ulimwengu.

Uzalishaji wa nyanya duniani na hapa Tanzania
Nchi zinazolima nyanya kwa wingi duniani ni pamoja na USA, Italia na Mexico. Kwa upande wa Africa nchi zinazo lima ni kama; Malawi, Zambia na Botswana.
Zao hili hulimwa pia katika nchi za Africa Mashariki, ikiwemo Kenya, uganda na Tanzania.

Zao la nyanya linalimwa karibu maeneo yote ya Tanzania. Uzalishaji wa nyanya ni mkubwa kuliko mazao mengine ya mbogamboga yanayolimwa hapa Tanzania, uzalishaji wa nyanya kwa mwaka ni jumla ya tani 129,578 ikiwakilisha asalimia 51 ya mazao yote ya mboga. Kwa mujibu wa Wizara ya kilimo ya Tanzania maeneo yanalolima sana nyanya ni pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro (Hai, Moshi na Rombo), Arusha (Arumeru), Morogoro (Mgeta), Tanga (Lushoto), Mbeya (Mbeya vijijini) na Singida.

Morogoro ndiyo inayoongoza kwa kilimo hichi ikiwa na wazalishaji wenye zaidi ya hekta 6,159 (ekari 15,398). Pamoja na kwamba eneo la uzalishaji linaongezeka kwenye maeneo mengi lakini uzalishaji wa nyanya bado ni mdogo sana.

Uzalishaji mdogo unasababishwa na kupungua kwa rutuba ya ardhi, upepo, joto, ukame. Sababu nyingine ni pamoja na ukosefu wa aina za nyanya zenye mavuno mengi amabazo zinahimili mazingira ya kwetu, wadudu, magonjwa na magugu.

Mazingira
• Hali ya Hewa:
Nyanya hustawi vizuri zaidi kwenye mazingira ya joto la wastani kuanzia nyuzi joto 18-27 sentigreti. Mvua nyingi husababisha mlipuko wa magonjwa ya ukungu kama vile Baka jani chelewa n.k.)

• Udongo:
Nyanya hustawi kwenye aina zote za udongo kuanzia udongo wa kichanga, mweupe wa tifutifu hadi udongo wa mfinyanzi, ili mradi uwe na mboji ya kutosha na usiosimamisha/tuamisha maji. Pia uwe na uchachu wa wastani yaani pH 6.0 - 7.0.

Aina za Nyanya
Kutokana na tabia ya ukuaji, nyanya zinagawanyika katika makundi mawili:
1. Aina ndefu ( intermediate) kwa mfano ANNA F1, Tebgeru 97. Aina hizi hufanya vizuri zaidi zinapopandwa ndani ya greenhouse. Uvunaji wake ni wa muda mrefu, zipo ambazo zinavunwa hata zaidi ya miezi 6, yaani hiyo miezi 6 ni ya uvunaji.
2. Aina fupi (determinate) kwa mfano Tanya, Cal J, Mwanga, Onyx, Roma VF (nyanya mshumaa)

Kotokana na uchavushaji, nyanya zinagawanyika makundi mawaili:
1. OPV (Open Pollinated Variety) - Aina za kawaida
2. Hybrid – Chotara: Hizi ni aina zenye mavuno mengi, kati ya hizo zipo aina fupi na ndefu.
Katika karne hii ya 21, nyanya zinazopendelewa kulimwa zaidi na wakulima, ni zile zinazoweza kuvumilia magonjwa, zinazo zaa sana, na zenye ganda gumu ili kufanikisha usafirishaji, na kuhifadhika kwa siku nyingi bila kuharibika mapema.

Kuandaa Kitalu cha Nyanya

Mambo muhimu ya kuzingatia:
• Kitalu kiwe karibu na maji ya kutosha na ya kudumu
• Kiwe sehemu iliyowazi na yenye udongo ulio na rutuba ya kutosha
• Eneo la kitalu kama ni kubwa liwe tambarare au na mwiinuko kidogo ili kuepuka maji yasituame kwenye kitalu, mtelemko ukiwa mkali sana nao sio mzuri kwani husababisha mmomonyoko wa udongo.
• Kitalu kiwe sehemu ambayo haikuwa na zao la nyanya au viazi mviringo (au mazao ya jamii ya nyanya k.m. mnavu, biringanya n.k.)
• Kiwe sehemu ambayo ni rahisi kupata huduma zote muhimu kwa urahisi, ikiwa ni pamoja na uhamishaji wa miche kwenda sehemu nyingine. Pia kurahisisha usambazaji wa miche kwenda sehemu nyingine.

Kuandaa Matuta ya Kusia Mbegu za Nyanya

Aina ya matuta:
– matuta ya makingo (sunken seed bed)
– matuta ya kunyanyulia udongo (raised seed bed)
– matuta ya kawaida (flat seed beds)

Mambo Muhimu ya Kuzingatia wakati wa Kuandaa Matuta
• Tuta liwe na upana kati ya sentimita 90-120, na urefu wowote, [ili mradi muhudumu anaweza kutoa huduma nyingine zote kitaluni bila kukanyaga miche].
• Kwatua/lima kina kirefu cha kutosha kiasi cha sentimita 15-20 ili mizizi iweze kusambaa vizuri ardhini.
• Choma takataka juu ya kitalu, au funika tuta kwa nailoni, majuma 4-8 ili kuua vimelea vya magonjwa na wadudu.
• Wakati wa kuandaa, kitalu, ongeza mbolea aina ya samadi/vunde au mboji kwenye udongo kisha kwatua ili ichanganyike vizuri na udongo.
• Changanya kiasi cha debe 1 hadi 2 kila baada ya mita moja (hatua moja) mraba.
• Tuta lisiwe na mabonde mabonde au mawe mawe ambayo yanaweza kuzuia usambaaji mzuri wa mbegu kwenye tuta, lisawazishwe vizuri ili kuhakikisha usambazaji mzuri wa mbegu na kuepuka mbegu kufukiwa chini mno kiasi ambacho hazitaota.

Faida na Hasara za Matuta yaliyotajwa hapo juu

1. Matuta ya kunyanyulia udongo (raised seed beds);
– matuta ya namna hii huruhusu maji, hewa na mizizi kupenya kwenye udongo kwa urahisi zaidi.
– Mazao ya mizizi hupata nafasi ya kutosha kutanuka haraka zaidi
– Matuta haya hayatuamishi maji kama mengine, hivyo hutumika zaidi kwenye maeneo yanayokuwa na mvua mara kwa mara.

Hasara:
o Matuta ya namna hii yana sababisha sana mmomonyoko wa udongo kama hayakutengenezwa vizuri.

2. Matuta ya makingo (sunken seed beds):
Faida:
· matuta haya ni rahisi kutengeneza
· hutumika wakati wa kiangazi ili kuhifadhi maji na unyevu
· nyevu mdogo unaopatikana ardhini
· ni rahisi kumwagilia kwa kutumia maji ya mfereji au bomba
· huhifadhi unyevu nyevu kwenye ardhi kwa muda mrefu
· huzuia mmomonyoka wa ardhi

Hasara:
· Matuta ya aina hii hayawezi kutumika kwenye maeneo yenye
· mvua nyingi.

3. Matuta ya kawaida (flat seed beds):
Faida:
· ni rahisi sana kutengeneza kwani udongo ukisha kwatuliwa
· na kusambazwa mbegu huoteshwa
· ni rahisi kutumia eneo kubwa kuotesha mbegu

Hasara:
Matuta ya aina hii hayawezi kutumika kwenye maeneo yenye mvua nyingi.

Kusia Mbegu
• Hakikisha ubora na uotaji wa mbegu kabla ya kuzipanda kitaluni (germination test)
• Weka mistari kwenye tuta kulingana na ukubwa wa tuta, lakini mistari isiwe chini au zaidi ya sentimita 15-20 toka mstari hadi mstari
• Kina cha mistari kisiwe cha kutisha bali kiwe kati ya sentimita 1-2
• Matuta yapate maji ya kutosha siku moja kabla ya kusia mbegu. Ni vizuri kutumia chombo cha kumwagilia (watering can).
• Mbegu ziatikwe kwenye mistari na zisambazwe vizuri ili kufanikisha usambaaji mzuri wa mbegu kwenye tuta. Changanya mchanga laini na mbegu kisha sambaza kwenye mistari iliyoandaliwa kwenye tuta.

Mbegu zinaweza pia kuatikwa kwenye tuta bila mistari, lakini zisambazwe kwa uwiano mzuri kwenye tuta ili kupunguza msongamano. Msongamano husabisha magonjwa ya fangasi kama vile kinyausi (damping off) au ukungu (blight).
• Weka matandazo kiasi cha kutosha ambacho hakitazuia kuota kwa mbegu.
• Mara baada ya kuatika mbegu, mwagilia maji kiasi cha kutosha kulingana na unyevu nyevu ulioko ardhini

Mambo ya Kuzingatia baada ya kusia mbegu pamoja na Matunzo Kitaluni
• Mwagilia maji kwenye kitalu baada ya kuotesha kulingana na unyevu nyevu uliopo kwenye udongo.
• Miche yote ikisha ota, ondoa matandazo, kisha weka chanja ili kupunguza mionzi ya jua ambayo inaweza kuunguza miche michanga. (kipindi cha baridi si muhimu sana)
• Punguzia miche (thinning) ili ibakie kwenye nafasi ya kutosha. Hivyo miche ibakie kwenye umbali wa sentimita 2.5 - 4. Hii itapunguza magonjwa ya ulemavu na mnyauko, pia itasaidia kupata miche bora na yenye nguvu.
• Endelea kumwagilia hadi miche ifikie kimo kinachofaa kuhamishia shambani.
• Punguza kiwango cha umwagiliaji maji, siku chache kabla ya kuhamishia miche shambani, yaani siku 7-10.

Kanuni na Mbinu za kuhamisha miche toka Kitaluni kwenda shambani (Transplanting
Rules)
• Mwagilia miche masaa machache kabla ya kuhamishia miche shambani ili wakati wa kung’oa miche mizizi ishikamane vizuri na udongo.
• Kabla ya kuhamisha miche, mashimo yawe yamekwisha andaliwa katika nafasi zinazo stahili huko shambani.
• Miche ihamishwe wakati wa jioni ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na jua.
• Kwa ujumla karibu mazao yote ya mboga mboga huwa tayari kuhamishiwa shambani yakiwa na majani kamili kati ya 2-6 pamoja na mizizi mingi iliyostawi vizuri.
• Mche lazima uwe na afya nzuri, uwe umenyooka vizuri, hivyo miche yote iliyonyongea au myembamba kupita kiasi isichukuliwe wakati wa kupeleka shambani.
• Ng’oa miche kwa uangalifu hasa pamoja na udongo wake kwa kutumia vifaa husika ili mizizi isidhurike.
• Miche ihamishiwe shambani mapema mara baada ya kung’olewa toka kitaluni.
• Wakati wa kuhamisha miche, uangalifu mkubwa utumike ili kutoharibu miche/mizizi.

Maandalizi ya Shamba la Nyanya
• Shamba la nyanya liandaliwe mwezi 1-2 kabla ya kupanda miche.
• Mara baada ya kulima choma nyasi juu ya udongo au ondoa magugu yote yanayoweza kuhifadhi wadudu na magonjwa ya nyanya.
• Siku moja au mbili kabla ya kuhamishia nyanya shambani, mwagilia sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kuhamishia nyanya.
• Nafasi kati ya mche hadi mche ni wastani wa sentimita (50-60) x (50-75) kutegemeana na aina au hali ya hewa. Kama ni kipindi cha baridi ni vyema nyanya zikapandwa mbalimbali ili kuruhusu mzungungo wa hewa na kuzuia magonjwa ya fangasi.

Jinsi ya kupanda miche:
• Hamisha miche toka kitaluni pamoja na udongo wake
• Sambaza mizizi vizuri kwenye shimo bila kukunja.
• Fukia miche kina kile kile ambacho shina lilikuwa limefukiwa bustanini.
• Mwagilia maji ya kutosha kulingana na unyevunyevu uliopo kwenye udongo kasha weka matandazo na kivuli ili kupunguza uharibifu unaosababishwa na mionzi ya jua.

Mambo muhimu ya kuzingatia baada ya kuhamishia Miche Shambani
• Kagua shamba mara kwa mara ili kujua maendeleo au matatizo yaliyoko shambani mapema
• Hakikisha shamba ni safi wakati wote, palilia shamba na hakikisha magugu yote hasa yale ya jamii ya nyanya yamelimiwa chini.
• Ondoa mimea iliyoshambuliwa na magonjwa au ondoa sehemu zilizoshambuliwa, kisha zifukiwe chini au kuunguza moto.
• Punguza matawi na vikonyo ili kuongeza mwanga wa kutosha kwenye nyanya pamoja na kuruhusu mzunguko wa kutosha wa upepo na kusababisha mazingira magumu ya wadudu maadui kwenye nyanya, hasa wale wanaopenda kiza na magonjwa yanayopendelea unyevunyevu.
Asante sana:

No comments:

Post a Comment