Friday, October 12, 2018

KILIMO BORA CHA NYANYA


Nyanya-zilizokomaa-zimeiva


Utangulizi


Nyanya ni zao la mboga linalolimwa sehemu nyingi duniani kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na pia kama zao la biashara. Nyanya ni aina ya mboga inayo zalishwa kwa wingi sana duniani. Kwa Tanzania, nyanya ni zao la kwanza katika mazao ya mboga linalolimwa na kuliwa kwa wingi ukilinganisha na mboga zingine. Nyanya hutumika karibu katika kila mlo. Kulingana na umuhimu wa zao hili kama chakula na pia kama zao linalomwingizia kipato mkulima, kuna haja ya kutoa mafunzo kuhusu mbinu bora za uzalishaji wake.



Maeneo yanayolima nyanya
Inadhaniwa kuwa asili ya nyanya ni nchi ya Peru au Equador huko Amerika ya Kusini. Mmea huu ulianza kuzalishwa kama zao katika nchi ya Mexico na baadaye kusambaa katika nchi nyingine za ulimwengu.

Nchi zinazolima nyanya kwa wingi duniani ni pamoja na USA, Italia na Mexico. Kwa upande wa Africa ni kama; Malawi, Zambia na Botswana. Zao hili hulimwa pia katika nchi za Africa Mashariki, ikiwemo Kenya, uganda na Tanzania.

Kwa upande wa Tanzania mikoa inayolima nyanya kwa wingi hasa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na biashara ni pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro (Hai, Moshi na Rombo), Arusha (Arumeru), Morogoro (Mgeta), Iringa (Ilula), Tanga (Lushoto), Mbeya (Mbeya vijijini) na Singida.

nyanya-zilizochumwa
Nyanya kwenye sahani

Mazingira yanayofaa kwa kilimo cha nyanya

Hali ya Hewa: Nyanya hustawi vizuri zaidi kwenye mazingira ya joto la wastani kuanzia nyuzi joto 18-27 sentigreti. Mvua nyingi husababisha mlipuko wa magonjwa ya ukungu kama vile Baka jani chelewa)

Udongo: Nyanya hustawi kwenye aina zote za udongo kuanzia udongo wa kichanga, mweupe wa tifutifu hadi udongo wa mfinyanzi, ili mradi uwe na mboji ya kutosha na usiosimamisha/tuamisha maji. Pia uwe na uchachu wa wastani yaani pH 6.0 - 7.0.

Mwinuko: Nyanya hustawi vizuri kutoka sehemu za mwambao hadi kwenye mwinuko wa mita 400-1500 kutoka usawa wa bahari; yaani nyanda za chini kati hadi za juu kutoka usawa wa bahari. Nyanya zinazopandwa nyanda za juu sana hukumbwa na mvua za mara kwa mara ambazo huambatana na magonjwa ya jamii ya ukungu; kama Bakajani chelewa (Late Blight)

Aina za nyanya

Kutokana na tabia ya ukuaji, nyanya zinagawanyika katika makundi mawili:
  1. Aina ndefu (intermediate) kwa mfano ANNA F1, Tengeru 97, Marglobe (M2009). Aina hizi hufanya vizuri zaidi zinapopandwa ndani ya greenhouse. Uvunaji wake ni wa muda mrefu, zipo ambazo zinavunwa hata zaidi ya miezi 6, yaani hiyo miezi 6 ni ya uvunaji.
  2. Aina fupi (determinate) kwa mfano Tanya, Cal J, Mwanga, Onyx, Roma VF (nyanya mshumaa)
Kulingana na uchavushaji, nyanya zinagawanyika katika makundi mawaili:
  1. OPV (Open Pollinated Variety) - Hizi ni aina za kawaida
  2. Hybrid - Chotara: Hizi ni nyanya zilizoboreshwa, aina hii zina mavuno mengi, kati ya hizo zipo aina fupi na ndefu.

Hata hivyo katika karne hii ya 21, nyanya zinazopendelewa kulimwa zaidi na wakulima, ni zile zinazoweza kuvumilia magonjwa, zinazo zaa sana, na zenye ganda gumu ili kufanikisha usafirishaji, na kuhifadhika kwa siku nyingi bila kuharibika mapema. Nyanya zinazoonyesha kuwa na sifa ya kuhifadhika bila kuharibika mapema ni kama:
a) Tengeru’97 ambayo ina sifa vifuatazo:
  • Huzaa sana kutokana na wingi wa matunda na muda mrefu wa kuvuna, ambao hufikia michumo mikubwa kati ya 6-7 kuanzia kuvuna hadi mwisho wa mavuno.
  • Aina hii ina sifa ya kuwa na ganda gumu, hivyo haziharibiki haraka wakati wa kusafirisha au kuhifadhi (wastani wa siku 20)
  • Zina sifa ya kuvumilia baadhi ya magonjwa kama vile ugonjwa wa kunyauka
  • Tengeru’97 hustahimili mashambulizi ya minyoo fundo (Root knot nematodes)
b) Tanya
  • Sifa kubwa ya Tanya ni kwamba nayo huzaa sana
  • Huwa na ganda/ngozi ngumu ambayo inazuia kuoza au kuharibika kwa urahisi wakati wa kusafirisha au wakati wa kuhifadhi kwa muda mrefu.
  • Tanya nayo ina ladha nzuri inayopendelewa na walaji wengi

Zingatia: Tatizo la Tanya na T97 ni kwamba si kubwa sana kama marglobe 2009. Lakini ukubwa ni karibu unge karibiana, haujapishana sana. Kwa ujumla, ukubwa na wingi wa mazao hutegemea sana matunzo, udongo, hali ya hewa na mazingira kwa ujumla.

Maandalizi ya Shamba la Nyanya

Shamba la nyanya liandaliwe mwezi mmoja au miwili kabla ya kupanda miche. Mara baada ya kulima choma nyasi juu ya udongo au ondoa magugu yote yanayoweza kuhifadhi wadudu na magonjwa ya nyanya. Siku moja au mbili kabla ya kuhamishia nyanya shambani, mwagilia sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kuhamishia nyanya. Andaa mashimo ya nyanya kutegemeana na idadi ya miche uliyonayo, nafasi na aina ya nyanya. Nafasi kati ya mche hadi mche ni wastani wa sentimita (50-60) x (50-75) kutegemeana na aina au zao litakalo changanywa na nyanya.


Jinsi ya kupanda miche ya nyanya
  • Weka samadi viganja viwili au gram 5 za mbolea ya kupandia kwenye shimo kabla ya kupanda mche.
  • Hamisha miche toka kitaluni pamoja na udongo wake
  • Sambaza mizizi vizuri kwenye shimo bila kukunja.
  • Fukia miche kina kile kile ambacho shina lilikuwa limefukiwa kitaluni.
  • Mwagilia maji ya kutosha kulingana na unyevunyevu uliopo kwenye udongo kisha weka matandazo na kivuli ili kupunguza uharibifu unaosababishwa na mionzi ya jua.
miche-iliyopandikizwa-shambani
Miche iliyopandikizwa shambani

Utunzaji wa zao la nyanya shambani

Umwagiliaji wa nyanya
Nyanya, kama ilivyo kwa mazao mengine, zinahitaji maji mengi ili kuzaa matunda yenye afya. Kutegemeana na aina ya udongo, unaweza kumwagilia nyanya mara mbili kwa wiki. Hakikisha unapanga ratiba maalum ya kumwagilia na unaifuata ili kuepuka kumwagilia kiholela holela kwani umwagiliaji usio na mpangilio huathiri afya ya matunda ya nyanya na kupelekea nyanya kuoza kitako (tomato blossom end rot). Unapotumia vifaa kama water can au mpira jitahidi sana usimwagilie kwenye majani ya mmea au matunda kwa sababu kulowesha mmea kunavutia wadudu na magonjwa ya ukungu unaoharibu nyanya.

Zingatia: usituamishe maji kwenye bustani au shamba la nyanya,

Palizi: Kudhibiti magugu
Hakikisha shamba ni safi wakati wote, palilia shamba na hakikisha magugu yote hasa yale ya jamii ya nyanya yamelimiwa chini. Palilia shamba lako wiki ya pili au ya tatu baada ya kupandikiza miche, lakini unaweza kupalilia kila unapoona magugu kwani shamba linatakiwa kuwa safi muda wote. Unaweza kuondoa magugu kwa kutumia dawa za kuua magugu au jembe la mkono. Magugu ni hatari kwa sababu tatu:

Kwanza: magugu yanashandana na mimea katika kuchukua nafasi na hivyo mimea kushindwa kujitanua. Pili: magugu huzuia mimea ya nyanya kupata mwanga wa jua wakutosha hivyo kuifanya mimea kushindwa kujitengenea chakula cha kutosha. Na tatu: magugu hushindana na mimea ya nyanya kufyonza virutubisho/chakula ardhini kitu ambacho kinapelekea mimea kuwa dhaifu. Pia magugu yanahifadhi wadudu na magonjwa na hivyo kuhatarisha zaidi usalama wa nyanya.

Mahitaji ya mbolea kwenye nyanya
  • Mbolea ya kupandia: weka mbolea ya DAP au Minjingu wakati wa kupandikiza miche shambani. Kiasi cha gram 5 ambayo ni sawa sawa na kifuniko kimoja cha soda kinatosha kwa kila shimo lenye mche mmoja. Tanguliza mbolea kwanza kwenye shimo kisha funika na udongo kiasi ili mbolea isigusane moja kwa moja na mizizi ya nyanya.

  • Mbolea ya kukuzia: unatakiwa kuongeza mbolea ya kukuzia kipindi cha wiki mbili au tatu baada ya kupandikiza miche shambani. Mbolea hii ya iwekwe kuzunguka shina la mmea kwa umbali wa sentimeta 5 kutoka kwenye shina. Kwa ajili ya kukuzia mimea ya nyanya tumia mbolea kama vile CAN, NPK, au SA. Tumia kifuniko kimoja cha soda kwa shina. Mbolea hii inaweza kuwekwa mara mbili kabla ya mvuno wa kwanza.


Ili kurefusha kupindi cha uzaaji wa zao la nyanya (na hata mazao mengine yatoayo matunda kama vile nyanya chungu, biringanya, na pilipili hoho) inapaswa kuongezea mbolea katika kipindi cha uvunaji mfano baada ya kuvuna mara mbili unashauriwa kuongeza mbolea ya samadi na mbolea kama vile NPK. Hii inasaidia mmea kuendelea kutoa maua bila kuchoka.

Kwa kawaida nyanya fupi jamii ya “Roma” huweza kuzaa na kuvunwa kwa kipindi cha wiki 6 hadi 8 tu. Lakini kama utakuwa unaongezea mbolea na kukazania matunzo ya shambani (hasa usafi wa shamba na kumwagilia maji ya kutosha), nyanya zinaweza kuendelea kuzaa kwa muda mrefu zaidi. Hii ni tofauti na mazoea ya wakulima wengi kuwa mara nyanya zianzapo kuzaa huduma za palizi na usafi wa shamba huachwa na kutilia maanani kazi ya kuvuna pekee. Hii inajitokeza zaidi kwenye aina ya nyanya fupi.

Kuweka matandazo
Matandazo ni nylon, majani au takataka za mimea zinazowekwa shambani au bustanini kwa lengo la kutunza unyevu na kuzuia au kupunguza kasi ya uotaji wa magugu, pia yakioza huongeza rutuba kwenye udongo. Mfano wa matandazo yanayoweza kutumika katika shamba la nyanya ni: nylon/turubai (plastic mulch), majani makavu, majani ya migomba, pumba za mazao, takataka za mbao. Plastic mulch inawekwa kabla ya kupandikiza miche shambani lakini matandazo mengine yawekwe baada ya kupandikiza miche. Na inafaa yawekwe kuzunguka eneo la shimo la mmea au katika shamba zima. Hivyo ni vizuri matandazo ya aina hii yawekwe mara tu baada ya kupandikiza (kama shamba halina magugu) au baada ya palizi ya kwanza.

shamba-lenye-matandazo
Matandazo kwenye shamba la nyanya


Kupogolea matawi
Punguza matawi na vikonyo ili kuongeza mwanga wa kutosha kwenye nyanya pamoja na kuruhusu mzunguko wa kutosha wa upepo na kusababisha mazingira magumu ya wadudu maadui kwenye nyanya, hasa wale wanaopenda kiza na magonjwa yanayopendelea unyevunyevu.

Kwa nyanya fupi ni vizuri kuhakikisha kuna matawi mengi iwezekanavyo ili kuweza kupata matunda mengi zaidi. Hivyo usipunguze matawi katika aina hii ya nyanya. Kwa nyanya ndefu zenye kuhitaji uegemezi, unashauriwa kukuza nyanya kwa tawi moja lisilo na vichipukizi pembeni au matawi mawili na kuacha mnyanya urefuke.

Kupogolea majani
Kupunguza majani ni muhimu pia katika kupunguza maambukizo ya ukungu katika shina na pia kutoa nafasi ili mwanga kupenya na kuruhusu mzunguko wa hewa. Kwa nyanya ndefu, majani ya chini ya matunda huondolewa kadiri unavyo endelea kuvuna.

Majani yapunguzwe kipindi cha asubuhi kwa kutumia mkono na siyo kisu kwani kinaweza kueneza magonjwa kutoka mche hadi mche. Ondoa majani yote ambayo yana dalili za magonjwa, yaliyozeeka, yaliyobadilika rangi na kuwa njano au kuanza kukauka. Wakati wa utoaji majani kuwa makini kutojeruhi shina kwani maambukizi yanaweza kuanzia hapo.

  • Kumbuka: Matawi/majani ya chini ya mmea wowote huwa hayana msaada sana katika uzaaji wa matunda na zaidi ni kwamba kwa kiasi kikubwa yamepoteza uwezo wake wa kutengeneza chakula. Hivyo kuendelea kubaki kwake kutapunguza chakula ambacho kingeenda kuongeza wingi na kukuza ukubwa wa matunda.

Kusimikia miti (staking)
Nyanya ziwekewe miti/mambo ili kuzuia zisianguke au kutambaa kwenye udongo, jambo ambalo linaweza kusababisha madhara mengi ya nyanya. Nyanya zinazotambaa zinahitaji kusaidiwa kuonyeshwa njia ili zisiguse chini. Nyanya zinapotambaa ardhini au kugusa chini zinaweza kuambukizwa wadudu na magonjwa ya ardhini kwa urahisi sana na pia wakati wa jua kali nyanya huchomwa na joto kali la ardhini. Hivyo basi shindilia mti mmoja (pigilia chini mambo) kando ya kila mmea wa nyanya na tumia kamba kufunga shina la mmea kwenye mti huo. Simika miti wiki mbili baada ya kupandikiza miche. Miti iwe imara na isiyooza haraka. Iwe na urefu wa mita moja hadi mbili na unene usiopungua sm 2.

Kusimikia-miti-nyanya
Shamba la nyanya lililosimkwa mambo



Uvunaji wa nyanya

Vuna wakati nyanya zimekomaa lakini bado zina rangi ya kijani. Wakati wa kuvuna nyanya tenganisha tunda na kikonyo chake na sio kikonyo na shina ili kuepuka kuujeruhi mmea kitu ambacho kinaweza hurahisisha maambikizi ya magonjwa kwa mimea. Wakati mzuri wa kuvuna ni asubuhi na jioni. Inatakiwa nyanya ziwekwe kwenye vyombo vinavyopitisha hewa, na vyombo maarufu ni matenga. Matenga ya nyanya yanaweza kuwa yametengenezwa kwa mbao au mianzi.

Mara tu baada ya kuvuna/kuchuma nyanya inashauriwa zikusanywe chini ya kivuli kwa muda ili ziweze kutoa joto la shambani kabla ya kuzifungasha kwenye matenga.

kuweka-nyanya-kwenye-matenga
Nyanya zinawekwa kwenye matenga

Namna ya kuhifadhi nyanya

Nyanya ni miongoni mwa mazao mepesi sana kuharibika hivyo ni muhimu sana nyanya zihifadhiwe mahali ambapo hapataharakisha kuoza kwake. Mahali pazuri ni pale penye ubaridi kiasi. Nyanya zenye ukijani zinaweza kuhifadhiwa mahali penye joto la 8o C hadi 10o C na zinaweza kukaa kwa muda wa hadi wiki tano bila kuharibika. Nyanya zilizoiva zinaweza kuhifadhiwa mahali penye kiasi cha joto cha 7o C na ni vizuri zaidi kama zitauzwa au kutumika mapema, yaani isizidi wiki moja. Katika mahali pakuhifadhia nyanya hali ya unyevu anga inatakiwa iwe ni kati ya 85% hadi 90%.


Hivi ndivyo tunavyohitimisha makala hii ya kilimo bora cha nyanya

No comments:

Post a Comment