Saturday, October 13, 2018

KILIMO BORA CHA UYOGA

 Uyoga upo wa aina mbalimbali hivyo usitawishaji wake hutofautiana katika mahitaji yake, ikiwa ni pamoja na hali ya hewa, malighafi za kuoteshea, urahisi wa teknologia ya kuotesha katika mazingira ya Tanzania na soko lake kwa wananchi na katika hotel. Uyoga unaozalishwa unafahamika. Aina zinazofaa kwa Tanzania ni zile ambazo hustawi vizuri, kwenye maeneo ya joto la wastani wa nyuzi joto 200C hadi 330C. Kwa mfano uyoga aina ya mamama

 Namna ya kuotesha Uyoga
Kabla ya kuanza kuzalisha uyoga inabidi kuwa na chumba chenye paa ambalo litazuia jua, mvua, na vumbi. Chumba hiki kinatakiwa kiwe na sakafu inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha utando wa uyoga. Mkulima wa kawaida anaweza kutumia kasha kama sehemu ya giza.

Hatua muhimu katika kuotesha uyoga

Hatua muhimu za kuotesha uyoga baada ya kupata mbegu ni kama ifuatavyo:

  • Kusanya masalia ya mzao kama vile mabua, majani ya mpunga, ngano, pumba za mpunga au mahindi, masalia ya miwa baada ya kukamua nk. Vitu hivi hutumika kama malighafi kwa kuoteshea uyoga.
  • Mabua, majani ya mpunga au migomba yakatwe kwa urefu usiozidi sm 6, au urefu wa vidole kwa kutumia panga au kisu.
  • Loweka mali ghafi kwenye maji ya kawaida kwa muda wa siku nzima (saa 24).
  • Kisha yachemshe kwa muda wa saa mbili ili kuua vijidudu pamoja na vimelea vilivyomo.
  • Ipua na umwage maji yote halafu tandaza kwenye kichanja kisafi ili yapoe bila kuchafuliwa na vumbi au vijidudu.
  • Kisha jaza mali ghafi hii katika mifuko ya nailoni tayari kwa kupanda mbegu.


Namna ya kupanda
Kuna aina mbili za upandaji

Aina ya kwanza
Chukua mfuko wa nailoni wenye upana wa sm 40 - 45 na kimo sm 75. Weka tabaka ya mali ghafi ya kuoteshea yenye kina cha sm 10 katika mfuko halafu tawanya mbegu ya uyoga juu yake. Baada ya kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya vioteshea na kuweka mbegu juu yake. Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka ifike ujazo wa robo tatu ya mfuko.

Aina ya pili
Changanya malighafi ya kuoteshea (baada ya kuchemshwa na kupoa) na mbegu ya uyoga katika uwiano wa 1: 25 (mbegu : malighafi ya kuoteshea) kwa uyoga aina ya mamama (Pleurotus spp.).
Kisha mchanganyiko huo ujazwe katika mifuko ya nailoni mifuko hii iwe na ukubwa wa sm 20 kwa sm 40 ambamo unaweza kujaza kilo 1 - 11/2 ya mali ghafi ya kuoteshea.
Funga mifuko na toboa matundu kwenye mifuko yenye kipenyo cha sm 1 kwa kila umbali wa sm 6 hadi 10 kwa kila mfuko. Matundu yawe mengi ili kuingiza hewa ya kutosha ndani ya mifuko. Kumbuka uyoga ni kiumbe hai hivyo unahitaji kupumua.

Matunzo ya zao la uyoga
Weka mifuko kwenye chumba cha giza. Kwa mkulima wa kawaida waweza kutumia kasha lisilopitisha mwanga kama chumba cha giza. Acha mifuko humo kwa muda wa siku 14 - 21 bila kufunua ili ukungu mweupe uweze kutanda vizuri. Utando wa uyoga ukishatanda vizuri kwenye mali ghafi ya kuoteshea, hamishia kwenye chumba chenye mwanga na hewa ya kutosha kisicho pigwa na jua. Katika chumba chenye mwanga, mifuko inaweza kuwekwa
kwenye, meza, chanja la waya au miti. Mifuko inaweza pia kuning’inizwa kwenye kamba toka kwenye boriti. Unatakiwa kudumisha hali ya unyevu kwenye chumba hicho cha mwanga kwa kumwaga maji sakafuni. Ukiona vipando vinakauka  unaweza kunyunyizia maji yaliyochemshwa na kupoa juu ya mifuko mara tatu au zaidi kwa siku.

Tumia bomba la mkononi lenye ukubwa wa lita moja kunyunyizia maji.
Tafadhali: usizidishe maji kwani maji yakiwa mengi sana yaweza kuozesha uyoga uliyoanza kuota. Aina nyingi za uyoga huanza kutoa vichwa (pini) siku 2 - 3 baada ya kuwekwa kwenye mwanga.

Uvunaji wa uyoga
Uyoga huwa tayari kuchumwa siku tatu baada ya vichwa /pini kuonekana. Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika katikati ya shina la uyoga kisha zungusha hadi uyoga ung’oke. Usiondoe kichwa peke yake katika kuvuna uyoga kwani kubakiza shina huzuia uyoga mwingine kutokea. Mkulima anatakiwa ajue soko la uyoga kabla ya kuvuna ili kuepuka gharama za kuhifadhi. Kwani uyoga ukishavunwa unatakiwa uliwe
kabla haujaharibika.

Jinsi ya kuhifadhi uyoga
i) Unaweza ukauweka uyoga kwenye mifuko ya karatasi na kuhifadhi kwenye jokofu.
ii) Unaweza ukauanika juani hadi ukauke na kuweka kwenye mifuko ya nailoni iliyofungwa vizuri ili isipitishe hewa na unyevu.

Mambo ya kuzingatia

  • Uzalishaji wa uyoga huzingatia sana hali ya hewa na vifaa ulivyonavyo, hivyo basi, kabla hujachagua aina ya uyoga unaotaka kupanda pata ushauri kwa wataalamu walio karibu nawe.
  • Ukishanunua mbegu, kama hupandi kwa muda huo, hakikisha umehifadhi mbegu hiyo kwenye jokofu. Kama huna jokofu la kuhifadhia, nunua mbegu baada ya kuandaa kila kitu. Hata hivyo, uotaji wa mbegu huwa mzuri kama zitakaa nje ya jokofu kwa siku mbili.
  • Mbegu za uyoga huwekwa ndani ya chupa yenye ujazo wa mililita 300, waweza kutumia chupa moja katika kupanda kwenye kilo 15 ya mali ghafi ya kuoteshea. Hakikisha unamaliza mbegu yote iliyo ndani ya chupa kwani ikibaki itapata maambukizo ya vimelea.
  • Hakikisha unaponunua mbegu iwe ni nyeupe. Mbegu ambayo siyo nyeupe ni dalili za maambukizo ya vimelea vingine na hivyo haifai kwa kupanda.
  • Hakikisha chumba cha kupandia ni kisafi na hakipati vumbi toka nje ili kuzuia maambukizo ya magonjwa ya uyoga. Usimwagilie uyoga maji yasiyochemshwa kwani maji hayo mara nyingi si salama. Yaweza kusababisha vimelea vingine kuota, kwani uyoga ni dhaifu kuhimili ushindani wa vimelea.
  • Pia waweza kusababisha magonjwa ya uyoga ambayo kutibu kwake kunahitaji kutumia dawa za viwandani ambazo ni sumu na hivyo kusababisha madhara kwa mlaji.

No comments:

Post a Comment