Monday, October 8, 2018

Kilimo Bora cha Vitunguu Maji na Uhifadhi Wake


Utangulizi
Vitunguu ni zao muhimu sana hapa Tanzania. Mikoa ya Arusha, Manyara, Iringa, Mbeya, Tanga, Singida na Kilimanjaro ni maarufu sana kwa kilimo cha vitunguu na ni zao la chakula na biashara kwa mkulima mdogo. Uzalishaji wa vitunguu bado ni mdogo (tani nne kwa hekta) na upotevu wa mazao baada ya kuvuna ni mkubwa (50 %– 80%) kutokana na hifadhi duni hivyo wakulima wanahitaji utaalamu wa kilimo bora na hifadhi ya vitunguu ili kuongeza uzalishaji na kipato.

Uzalishaji wa vitunguu
Zao la vitunguu linazalishwa kutokana na mbegu na miche inakuzwa kwenye kitalu kabla ya kupandikizawa shamban. Miche inakuwa na kuzaa vitunguu.Vitunguu vikikomaa, vinavunwa na kuhifadhiwa vikiwa katika hali ya kulala bwete. Katika hali hii vitunguu vinaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu aitha kwa ajili ya kuzalisha mbegu msimu unaofuata au kuuza. Wingi na ubora wa zao la vitunguu hutegemea; hali ya hewa, aina ya vitunguu, upatikanaji wa mbegu bora, kilimo bora, uangalifu wakati wa kuvuna, usafirishaji na hifadhi bora.

Hali ya hewa na maji
Hali ya hewa na maji ni vipengele muhimu sana vya kuzingatia katika uzalishaji wa vitunguu. Vitunguu vinastawi vizuri katika hali ya ukavu kwa kutumia umwagiliaji. Maji mengi hasa wakati wa masika inasababisha magonjwa mengi hasa ukungu, vitunguu haviwezi kukomaa vizuri, hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mazao. Jua na hewa kavu ni muhimu sana wakati wa kukomaa na kuvuna vitunguu.

Aina za vitunguu
Aina bora za vitunguu ni pamoja na Mang’ola red, Red creole na Bombay Red. Hizi ni mbegu bora ambazo zinatoa mazao mengi kuanzia 40-60kgs kwa hekta ikiwa kilimo bora kitazingatiwa.Mkulima anaweza kuchagua mbegu kwa kuzingatia:-
  • Mahitaji ya soko (vitunguu vyekundu hupendwa zaidi)
  • Msimu wa kupanda
  • Uwezo wa kuzaa mazao mengi
  • Uwezo wa vitunguu kuhifadhiwa kwa muda mrefu.
Mbegu bora
Ubora wa mbegu ni muhimu sana, kwani ndiyo chanzo cha mazao bora. Mbegu bora inatoa miche yenye afya na kuzaa mazao mengi na bora. Mbegu za vitunguu inapoteza uoto wake upesi baada ya kuvunwa (mwaka1). Mbegu nzuri zina sifa zifuatazo:-
  • Uotaji zaidi ya 80%
  • Mbegu safi zisiyo na mchanganyhiko
  • Zimefungwa vizuri kwenye vyombo visivyopitisha hewa na unjevu.
Hivyo mkulima anaponunua mbegu za vitunguu azingatie yafuatayo:
  • Chanzo cha mbegu
  • Tarehe ya uzalishaji
  • Tarehe ya kuisha muda wake
  • Kifungashio cha mbegu.
Inashauriwa mkulima asipande mbegu zenye umri zaidi ya mwaka mmoja
Mbegu bora za vitunguu zinauzwa na makampuni binafsi kama: ALPHA Seed Co., Popvriend, Rotian Seed, Kibo Seed, East African Seed Company nk. Wasambazaji wa mbegu ni pamoja na maduka ya TFA, na maduka ya bembejeo za kilimo katika maduka mbalimbali.

Jinsi ya kuandaa kitalu na kuzalisha miche
  • Sehemu ya kitalu iwe wazi, mbali na kivuli na kiwe karibu na chanzo cha maji.
  • Tengeneza tuta la kubwa wa 1m x 2m . Urefu na idadi ya matuta hutegemea kiasi cha mbegu. Kiasi cha mbegu kwa hectare moja ni kilo 6 au 2 kg kwa eka.
  • Weka samadi iliyooza vizuri kiasi cha debe moja au mchanganyiko wa mbolea ya TSP na CAN (200gm) kwa uwiano wa 1:1 kwenye tuta changanya vizuri na udongo.
  • Sia mbegu kwenye mistari kwa nafasi ya 1 sm x 20 sm. Tawanya mbegu vizuri wakati wa kusia ili miche isisongamane.
  • Funika mbegu na weka matandazo ya nyasi kavu juu ya tuta na mwagiliwa maji. Udongo unatakiwa kuwa na unyevu kiasi mpaka mbegu ziote.
  • Nyasi ziondolewe mara tu mbegu zikiota (siku7-10 kutegemea hali ya hewa).
  • Miche itunzwe vizuri na kitalu kiwe katika hali ya usafi.
  • Miche imwagiliwe maji mpaka ifikie umri wa kupandikiza shambani (wiki 5-6)
Matatizo ya miche kitaluni ni kama yafuatayo:
Kuonza kwa mbegu, kunyauka kwa miche kabla na baada ya kuoto. Hali hii inasababishwa na ugonjwa wa ukungu “Kinyausi” .Dawa za ukungu kama Dithane M45 au Ridomil MZ nk zinatumike kuzuia (changanya dawa na povu la sabuni ili dawa ijishike kwenye majani). Pia uangalifu uwepo wakati wa kumwagilia maji. Mwagilia maji wakati wa asubuhi au jioni. Epuka kumwagilia maji wakati wa jua kali kwani unjevunjevu hewani unaongeza na kusababisha vimelea vya magonjwa. Wadudu waharibifu ni pamoja na Chawa wekundu.ambao wanashambulia majani, Sota ambao hukata miche. Dawa za viwandani kama Thiodan , Selecron au Dusrban zinazuia na kudhibiti hwa wadudu.

Baada ya wiki 5 au 6, kutegemeana na hali ya hewa miche itakuwa tayari kupandikiza shambani. Miche iimarishwe kwa kusitisha maji, wiki moja kabla ya kupandikiza.
Kutayarisha shamba
Shamba litayarishwe sehemu usiyokuwa na mwinuko, sehemu ya wazi ambayo haijalimwa vitunguu kwa muda wa miaka 2 -3. Shamba liwe karibu na chanzo cha maji kwa ajili ya umwagiliaji. Matuta 1m x 3m au majaruba ya 2mx 3m.yanafaa kwa kupanda miche. Matatu au majaruba yanarahisisha umwagiliaji, palizi na unyunyiziaji wa dawa.

Kupandikiza miche shambani na matumizi ya mbolea
Weka samadi debe 2 au mbolea ya TSP au DAP kwenye tuta au jaruba na kuchanganya na udongo. Mbolea kiasi cha mifuko 2 TSP au DAP kwa hekta au ¾ mfuko kwa eka moja inashauriwa. Chagua miche yenye afya, majani na mizizi ya ipunguzwe ili kurahisisha upandaji. Panda miche kwenye mistari kwa nafasi ya sm 20 toka mstari hadi mstari, na miche hadi mche kwa nafasi ya sm 8 au sm 10. Tumia kijiti au kitu chochote chenye ncha kuchimba vijishimo vya kupandia miche. Mwagilia maji ya kutosha kila siku hasa sehemu zenye jua kali. Mbolea ya kukuzia CAN kiasi cha mifuko 2 kwa hekta au ¾ mfuko kwa eka moja iwekwe wiki mbili baada ya kupandikiza miche. Matumizi ya mbolea ya CAN yanataka uangalifu sana. Mbolea ikizidi hufanya mimea kuwa teketeke, shingo ya vitunguu kuwa nene, kuchelewesha kukoma na kupunguza mazao na ubora wa vitunguu. Pia kuoza kwa vitunguu ghalani kunaongezeka

Kuzuia magugu
Miche ya vitungguu, huota taratibu sana, hivyo miezi ya mwanzoni, miche husongwa sana na magugu. Palizi mbili mpaka tatu zinashauriwa na zinatosha kuweka shamba safi. Matumizi ya dawa za magugu ni madogo lakini dawa zinazoshauriwa ni pamoja na Alachlor na Oxyflourfen (Goal 2E). Hizi dawa ni nzuri kwani zina uwezo wa kuua magugu aina mbalimbali. Dawa inapuliziwa wiki mbili mpaka tatu baada ya kupandikiza miche shambani. Palizi baada ya kutumia dawa ya magugu ni muhimu ili kuondoa magugu sugu na pia kutifulia vitunguu. Wakati wa palizi, vitunguu na mizizi iliyowazi ifunikwe kwa udongo ili kuzuia jua lisiunguze mizizi au kubabua vitunguu.

Magonjwa na wadudu waharibifu
Vitunguu vinashambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali na kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo kwanza shamba likaguliwe mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua hatua za kuzuia kabla uharibifu mkubwa haujatokea.

Magonjwa
a) Baka zambarau (Puple Blotch)
Ungonjwa huu unasababishwa na kuvu (fangasi). Chanzo kikubwa cha ugonjwa ni mbegu zenye ugonjwa. Pia ugonjwa unajitokeza wakati kuna ukungu na unyevunyegu mwingi hewani hasa wakati wa masika. Kiasi cha 60-80 % ya mazao yanaweza kupotea kama ugonjwa hautadhibitiwa. Dalili za ugonjwa ni:-
  • kujitokeza madoa meupe yaliyodidimia kwenye majani na kwenye mashina ya mbegu
  • rangi ya zambarau kuwepo katikati ya doa jeupe.
  • majani kuanguka
  • mashina ya mbegu kuanguka kabla ya mbegu kutengenezwa
Njia za kudhibiti:-
  • kupanda mbegu safi
  • kupanda vitunguu kwa kutumia mzunguko wa mazao
  • kuteketeza msalii ya vitunguu baada ya kuvuna
  • kupulizia dawa zilizopendekezwa kama Dithane M45 na Ridomil MZ. Dawa hizi zinachanganywa na povu la sabuni ili zijishike kwenye majani.
b) Ubwiri vinyoya (Downy Mildew)
Ugonjwa huu unasababishwa na kuvu (fangasi) na kuenezwa na mbegu, hewa na masalia ya vitunguu. Unajitokeza wakati kuna unyevunyevu mwingi hewani hasa wakati wa masika na dalili zake ni kama zifuatazo:-
  • madoa yenye umbo la yai, rangi ya njano iliyofifia hujitokeza kwenye majani makukuu na kusambaa mpaka kwenye majani machanga.
  • baada ya siku chache madoa ya njano yanafunikwa na ukungu wa rangi ya kijivu.
  • majani yanasinyaa na kufa kuanzia kwenye ncha.
  • shina la mbegu huzungukwa na vidonda na kusababisha kichwa cha mbegu kuanguka.
Njia za kudhibiti ugonjwa ni kama zifuatavyo:-
  • kupanda mbegu safi
  • kupanda vitunguu kufuata mzunguko wa mazao
  • kupulizia dawa za ukungu kama dithane m45 na ridomil mz.
  • kuweka shamba safi
  • kuteketeza mabaki ya vitunguu
  • kumwagiliaji maji nyakati za asubuhi au jioni
c) Kinyausi (Damping – off)
Ugonjwa huu unasababishwa na fangasi na kuenezwa na udongo, mbegu na masalia ya mazao. Ugonjwa huu unasababisha mbegu kuoza kabla ya kuota na kunjauka kwa miche baada ya kuota. Ugonjwa unajitokeza hasa kitaluni ikiwa hali ya hewa ina unyevunyevu na udongo una maji maji.
Njia za kudhibiti ni kama zifuatazo:-
  • mbegu ziwe safi na ziwekwe dawa ya thiram
  • kutumia mzunguko wa mazao
  • kusia mbegu kwa nafasi za kutosha
  • kuepukana na kubananisha miche kitaluni
  • kuepukanana na kumwagilia maji wakati wa jua kali au wakati kuna ukungu
d) Virusi njano vya vitunguu (Onion yellow Dwarf virus)
Ugonjwa huu unasababishwa na virusi na kuenezwa na wadudu aina ya vidukari (wadudu mafuta). Dalili za ugonjwa ni:-
  • mistari ya rangi ya manjano kwenye majani.
  • kujikunja kwa majani
  • majani kugeuka rangi ya manjano na kuanguka
  • mimea mzima kudumaa, kujikunja na kufa.
Njia za kudhibiti ugonjwa huu ni:-
  • kutumia mbegu safi
  • kuweka shamba katika hali ya usafi
  • kuzuia wadudu kwa kupulizia dawa kama selecron, actellic, dursban nk.
Wadudu
Wadudu wanaosababisha uharibifu mkubwa kwenye vitunguu ni chawa wekundu (thrips) na sota (cutworms). Wadudu wengine ni pamoja na utitiri wekundu (red spider mites) na vipekecha majani (leaf miner)

a. Wadudu chawa (thrips)
Uharibifu uletwao na wadudu chawa, unatofautiana msimu mmoja na mwingine kutegemeana na hali ya hewa. Mvua kidogo pamoja na joto kali unasababisha mlipuko wa wadudu. Wanshambulia majani kwa kukwaruakwarua na kunyonya maji hivyo kusababisha majani kuwa na rangi ya fedha/siliver na baadaye majani yanakauka. Upungufu mkubwa wa mazao unatokea.
Njia ya kudhibiti hawa wadudu ni:-
  • kuweka shamba katika hali ya usafi
  • kuondoa magugu shambani na yanayozunguka shamba la vitunguu
  •  kupulizia dawa ya wadudu kama karate, selecron, dursban, actellic.
b. Sota (Cutworms)
Sota au viwavi wa nondo wanasababisha uharibifu mkubwa. Viwavi wanakata mashina ya miche michanga sehemu ya chini ya shina juu ya ardhi. Sota wanapendelea kula wakati wa usiku na mchana kujificha kwenye ardhi karibu sana na sehemu waliokata shina. Uharibifu huu unapunguza sana idadi ya mimea shambani na kuleta upungufu wa mazao.  Wadudu hawa wanadhibitiwa kwa kupulizia dawa kama; Karate Dursban na Actellic na kuweka shamba katika hali ya usafi.

c. Utitiri wekundu (Red spider mites)
Hawa ni wadudu wadogo sana, ambao wanajificha upande wa chini wa majani. Wanafyonza maji maji kwenye majani na kusababisha majani kuwa na rangi nyeupe. Wadudu hawa wanatengeneza utando mweupe kuzunguka majani na mashina. Mmea unashindwa kutengeneza chakula na baadaye inakufa.
Njia ya kudhibiti:
  • kupulizia dawa za wadudu Karate na Selecron.
  • kuteketeza masalia ya mazao
  • kutumia mzunguko wa mazao
d. Vipekecha majani (leaf miner)
Hawa ni aina ya inzi wadogo, ambao viwavi wake wanashambulia majani, kwa kupekecha na kutengeneza mitandao wa mitaro kwenye majani. Viwavi wanashambulia majani na kusababisha majani kukauka. Upungufu mkubwa wa mazao hutokea.
Njia ya dhibiti:
  • kupulizia dawa ya wadudu kama karate Selecron na Dursban
  • kuteketeza masalia ya mazao
  • kutumia mzunguko wa mazao
Kuvuna na hifadhi ya vitunguu
Kabla ya kuvuna vitunguu kagua shamba ili kuhakikisha kuwa vitunguu vimekomaa.

Dalili ya vitunguu kukomaa ni:-
  • majani kunyauka na kuanza kukauka
  • asilimia 75 -100% kuangusha shingo na majani kukauka.
Kuvuna
Vitunguu vinavunwa kwa mikono. Mimea inangolewa au kuchimbuliwa kwa kutumia rato (jembe uma). Baada ya kuvuna vitunguu vinaweza kuachwa shambani vikiwa vimefunikwa na majani kukinga jua kali kwa muda wa siku mbili au tatu kutegemeana na hali ya hewa. Lengo ni kuimarisha ngozi ya vitunguu na kufanya michubuko na majeraha madogo madogo yanayotokea wakati wa kuvuna kuwa magumu na kutengeneza mokovu ambayo yanazuia vimelea vya magonjwa kuingia ndani. Pia kupunguza unyevu kwenye majani na mashina na kuruhusu sehemu ya chini ya shingo kufunga. Ikiwa usalama ni mdogo, vitunguu vinachambuliwa na kukatwa majani na mizizi na kuanikwa sehemu nyingine.

Kuchambua
  • Tenga vitunguu vilivyooza, kuchubuka na kupasuka. Vitunguu vizuri vikaushwe peke yake.
  • Iwapo vitunguu vitahifadhiwa kwa kuninginiza kwenye chaga, basi shingo zisikatwe, bali zisukwe na kufungwa pamoja, na kuninginizwa
Kukausha
Hatua hii ni muhimu ili kupunguza unyevu, kufanya vitunguu viwe vigumu na kuwa katika hali ya kulala bwete.Vitunguu vinaweza kukaushwa kwa kuninginiza kwenye chaga zilizopangwa mfano wa dari ndani ya banda au kutandaza kwenye kichanja chenye kuruhusu mzunguko wa hewa pande zote, chini ya kivuli sehemu kavu. Epuka kukausha vitunguu chini kwenye aridhini na hasa sehemu zenye jua kali. Jua linababusha vitunguu na kusababisha uharibifu. Ukaushaji huchukua muda wa siku 7 au zaidi kutegemeana na hali ya hewa.

Kupanga madaraja
Vitunguu vinachambuliwa tena baada ya kukausha ili kuondoa vitunguu vyote vyenye ugonjwa au dalili za ugonjwa, vilivyoota na kutoa mizizi na vyenye shingo nene. Vitunguu vinapangwa kwenye madaraja mbalimbali kufuata ukubwa, umbo au rangi. Hii inawezesha kuapta soko zuri na kuepukana na upotevu mkubwa wakati wa kuhifadhi.

Kufungasha na kuweka vitambulisho
Vifungashio vinavyopatikana ni mifuko ya nyavu vyenye uwezo wa ujazo wa kilo 20 au magunia ya katani. Mifuko ya nyavu ina ujazo mdogo na pia inarahisisha ubebaji. Magunia ya katani yanatumika lakini yanaficha vitunguu visionekane pia vinachukua mzigo mzito na kuleta usumbufu wakati wa kupakia na kupakua. Vitambulisho vinawekwa kwenye vifungashio ili kusaidia wasafirishaji kujua mzigo ulikotoka na pia kutangaza bidhaa inayohusika kwenye masoko ya nje na ndani. Kwa soko la nje vitambulisho vinatakiwa na habari zifuatazo: 
  • Jina la bidhaa mf. Vitunguu Mango’la Red
  • Uzito kamili mf. 20 kg
  • Jina na anwani ya mkulima au kikundi, jina na anwani ya msafirishaji
  • Jina la kijiji wilaya, Mkoa na nchi mf. Igurusi, Mbarali, Mbeya, Tanzania
  • Grade 
Kwa soko la ndani vitambulisho vinakuwa na habari zifuatazo:
  • Jina la bidhaa.mf.vitunguu Mango,la Red
  • Uzito kamili mf. 20 kg
  • Jina la mkulima au kikundi na anwani Jitegemee, Box 20, Mbarali Mbeya
  • Jina na anwani ya msambazaji mf:Mr. Saidi Mbaga Box 70, Mbeya
Kusafirishaji
Uangalifu wakati wa kupakia, kusafirisha na kupakua ni muhimu ili kuepukana na uharibifu na upotevu wa vitunguu. Mara nyingi vitunguu vinaharibika kutokana na ujazo kupita kiasi kwenye vifungashio na vyombo vya usafiri, pia kutokana na upakiaji na mpangilio mbaya, ambao unasababisha ugandamizaji na kubonyea kwa vitunguu. Wakati wa usafirishaji yafuatayo yazingatiwe:-
  • kutumia vyombo vya usafiri vinavyofaa hasa magari yenye nafasi ya kutosha na yenye kupitisha hewa
  • kupanga mifuko katika tabaka zenye safu zisizodi tatu
  • mifuko isitupwe wakati wa kupakia na kupakua
  • vitunguu visichanganywe na mazao mengine.
Kuhifadhi
Vitunguu vinahifadhiwa kwenye maghala bora kama kribu au mabanda ambayo yanaruhusu hewa na paa kuezekwa kwa manyasi ili kupunguza joto.

Hifadhi kwenye kribu
Kribu inajengwa kwa fito au mianzi na kuinuliwa juu mita moja toka usawa wa aridhi. Upana wa kribu uwe kati ya sm 60 na 150 ili kuruhusu upepo kupita kwa urahisi. Upepo unaondoa unyevu na joto kwenye vitunguu. Kribu igawanywe sehemu mbili zenye kina cha sm 60 kila moja na kutenganishwa na uwazi was m 30, ili kuruhusu mzunguko wa hewa. Wakati wa kutengeneza kribu yaafutayo yazingatiwe:-
  • Kribu ijengwe kwenye sehemu yenye upepo
  • Kribu iezekwe kwa nyasi ili kudhibiti joto na jua
  • Miguu ya kribi iwekwe vizuizi vya panya.
  • Weka vutunguu tabaka mbili na kina cha vitunguu kisizidi sm 60
Hifadhi kwa kuninginiza vitunguu kwenye banda
Hili ni banda lenye uwazi mkubwa, lenye upana usiozidi mita tano, na urefu toka chini hadi juu usizidi mita 2½. Banda linajengwa kwa miti, fito, mbao au mianzi na vitunguu vinahifadhiwa kwa kuninginiza kwenye fremu za fito ndani ya banda. Safu za vitunguu hupangwa kufuata urefu wa banda na kimo cha banda. Urefu wa banda huelekezw a kwenye mkondo wa upepo ili kuruhusu upepo kuingia na kutoka. Banda liezekwe kwa nyasi ili kudhibiti joto na jua. Kribu au banda vinahifadhi vitunguu vizuri kwa muda wa miezi sita bila kuharibika.

Upotevu wa vitunguu ghalani
Vitunguu vingi hupotea wakati wa kuhifadhi kwa sababu ya:-
  • Kuoza
  • Kuota (toa majani na mizizi)
  • Kupoteza uzito
Kuoza
Kuoza kwa vitunguu vikiwa ghalani kunasababishwa na vimeliea vya fangasi au bacteia. Joto pamoja na unyevunyevu ndani ya ghala, kunasababisha kuzaliana na kuongezeka kwa vimelea vya magonjwa
Kudhibiti:
  • Weka ghala katika hali ya usafi, kausha vizuri na chambua vitunguu ili kabla ya kuhifadhi.
a ) Muozo Kitako (Bottom rot or basal rot)
Vimelea vya aina ya fungus vinavyoishi kwenye udongo, vinashambulia sehemu ya chini ya vitunguu. Vimelea vinapenya kwenye sehemu zenye michubuko, inayotokea wakati wa palizi, kuvuna au kusafirishwa. Vitunguu vinaoza na baadaye vinakauka na kusinyaa. Njia zifuatazo zinadhibiti:-
  • mzunguko wa mazao
  • kuchambuaji mzuri kabla ya kuhifadhi
  • kuepuka michubuko wakati wa palizi na kuvuna
b) Ukungu mweusi (Black mould).
Ugonjwa huu unaletwa na vimelea vya fangasi, vinavyoishi kwenye udongo. Vimelea vinazaliana katikati ya maganda na ukungu mweusi kama poda unaonekana. Baadaye maganda yanasinyaa na kuvunjika.
Kudhibiti
  • kutumia mzunguko wa mazao
  • kukagua ghala mara kwa mara na kuondoa vitunguu vilivyooza
  • kuweka ghala katika hali ya usafi.
  • Kuondoa masalia ya vitunguu na kuchoma moto.
c) Kuoza shingo (Neck rot)
Vimelea vya fangasi vinashambulia vitunguu vikiwa shambani kabla ya kuvuna. Ugonjwa hauonekani mpaka vitunguu vikomae, vivunwe, vikaushwe na kuhifadhiwa ghalani, ndipo ugonjwa hujitokeza. Ugonjwa unasababisha kuoza kwa vitunguu. Maganda ya vitunguu yanalainika kuanzia shingoni na nyama ya kitunguu huwa na sura ya maji maji. Vitunguu vilivyooza vinyauka na kusinyaa.
Kudhibiti;
  • kukausha vitunguu vizuri kabla ya kuhifadhi
  • kuchoma na kuharibu masalia ya vitunguu shambani na ghalani.
d) Muozo laini (Bacterial soft rot)
Ugonjwa unasababishwa na vimelea vya bacteria. Dalili kubwa ya ugonjwa huu ni kulainika kwa vitunguu na kutoa harufu mbaya. Ukiminya kitunguu maji yenye harufu mbaya yanatoka kwenye shingo. Muozo laini unatokea wakati hali ya hewa ikiwa na unyevunyevu na jotoi. Pia vitunguu vyenye shingo nene ambavyo havijakauka vizuri ni sehemu nzuri sana ya vimelea kuzaliana.
Kudhibiti :
  • Ukaushaji wa haraka na wa uhakika baada ya kuvuna unapunguza sana ugonjwa huu
 Kuota na kupoteza uzito wa vitunguu
Vitunguu vinakuwa katika hali ya kulala bwete bila kuota kwa zaidi ya miezi sita ikiwa hali ya hewa ghalani ni nzuri. Unyevunyevu mwingi ghalani ni adui mkubwa wa vitunguu vilivyohifadhiwa kwani inasababisha kuota kwa majani na mizizi. Pia hewa ikiwa kavu sana vitunguu hupoteza maji upesi na kusinyaa. Kuongezaka kwa joto na unyevunyevu ndani ya ghala kutokana na mzunguko mbaya wa hewa, uchafu ghalani, ukaushaji na uchambuaji mbaya vinasababisha uharibifu kubwa wa vitunguu ghalani
Kudhibiti ;
  • ghala liwe safi pia liwe na uwezo wa kupitisha hewa kavu na ubaridi wa kutosha.
  • ghala lijengwe sehemu yenye upepo na kuruhusu mzunguko mzuri wa hewa.
  • vifungashio vya vitunguu vipangwe vizuri ili kuruhusu hewa kupita juu na chini.
  • vitunguu ndani ya kribu/ghala vijazwe kina cha sentimeta 30-50.
  • vitunguu vichambuliwe vizuri kabla ya kuhifadhi.
  • vitunguu ghalani vikaguliwe mara kwa mara ili kuondoa vitunguu vilivyoharibika
Uuzaji wa vitunguu
Watu wa aina mabalimabali wanahusika na ununuzi na uuzaji wa vitunguu wakiwa ni pamoja na: wakulima, wachuuzi, wafanya biashara ndogondogo, wauza jumla, wauza rejareja, wasafirishaji na madalali. Ili koboresha uuzaji na kipato ni muhimu kuzingatia yafuatayo: 
  • Kuboresha ujazo kwa kufuata vipimo vinavyokubalika (kufuta lumbesa
  • Kupeana habari za masoko na bei.
  • Kuboresha usafirishaji kwa kutumia vikundi.
  • Kuwepo na mtiririko wa kuuza vitungu mwaka mzima, kwa kuboresha hifadhi ikiwa ni pamoja na maghala.
  • Kutathimini na kuzingatia ubora wa vitunguu.
  • Kutathimini na kuboresha ufungashaji na usafirishaji

1 comment:

  1. Nashukuru na nimefurahia hiyo article nlikuwa naomba namba za simu kwa ajili ya maswali kidogo ya mwongozo mzuri

    ReplyDelete