Mtama
unaweza kutumika kwa kuchemshwa na kuliwa kama ulivyo, kusagwa na
kutumika kwa uji, kutengenezea vinywaji kama vile bia, kuoka mikate, na
aina nyinginezo za vitafunwa. Mmea wa mtama pia hutumika kwa ajili ya
malisho ya mifugo kama vile hay na sileji. Mtama unastawis vizuri
kwenye mazingira yenye wastani wa milimita 400 – 700 za mvua kwa mwaka.
Pia mtama unavumilia sehemu zinazotuhamisha maji, na unaweza kulimwa
sehemu zenye mvua nyingi.
Mtaama
unafaa pia kwa sehemu kame zenye wastani wa joto la chini kiasi cha
nyuzi joto 18°C, ili kuweza kuota vizuri, na kiasi cha nyuzi joto
25-30°C ili kukua vizuri. Mtama hauwezi kuvumilia barafu. Mtama unaweza
kukua kwenye aina zote za udongo. Kwa kiasi kikubwa unafaa zaidi kwenye
udongo wa mfinyanzi, lakini pia kwenye udongo ambao una kiasi kidogo cha
mchanganyiko wa kichanga. Mtama unaweza kuvumilia uchachu kwenye udongo
kuanzia pH 5.0-8.5, na inavumilia udongo wenye chumvi kuliko yalivyo
mahindi.
Aina za mtama
Kwa
jumla kuna aina zaidi ya 30 za mtama zinazolimwa kama chakula. Mtama
hustawi vizuri kwenye joto ikivumilia pia ukame. Hivyo ni nafaka muhimi
kwenye maeneo yabisi za Afrika. Katika miaka ya nyuma kilimo chake
kiliachwa mara nyingi kwa ajili ya mahindi kwa sababu mahindi huleta
mazao makubwa zaidi kwa ekari. Lakini wakati wa ukame mahindi ni hasara
na watu hurudi-rudi kwenye kilimo cha mtama.
Aina
za mtama zinatofautiana kulingana na rangi zake, kuna nyeupe, nyekundu,
na kahawia. Mbegu za asili huwa zinachavushwa kwa urahisi zaidi lakini
mavuno yake huwa ni hafifu ukilinganisha na mbegu za kisasa. Hata hivyo,
aina za kisasa zinazalishwa kwa gharama nafuu zaidi zinapopandwa kwa
kufuata kanuni za kilimo bora.
Serena: Ina
punje za kahawia. Aina hii hustawi kwenye eneo lenye mvua za wastani na
hukomaa katika kipindi cha siku 110. Aina hii huwa na shina na mizizi
imara, ambapo huweza kuzalisha kiasi cha kilo 3,000 kwa hekari moja.
Ambapo zinahitajika kilo 5 za mbegu kwa hekari moja. Aina hii ina uwezo
wa kukabiliana na ugonjwa milia, kutu, na madoa ya kahawia kwenye
majani.
Seredo: Hii
ni aina nyingine yenye punje za kahawia, na inapendekezwa Kulimwa
kwenye eneo lenye mwinuko wa mita 1,500 kutoka usawa wa bahari. Aina hii
huchanua baada ya siku 71 na hukomaa katika kipindi cha siku 120. Aina
hii huwa ni ndefu, na ina uwezo wa kuzalisha kilo 5000 kwa hekari moja.
Ina uwezo wa kukabiliana na ugonjwa wa milia, kutu, mabaka kwenye
majani, na madoa ya kahawia kwenye majani.
Gadam: Inafanya
vizuri katika sehemu ambazo si kame sana. Katika nchi nyingi mfano
Kenya, aina hii ya mtama hutumika kutengenezea bia na pia kwa chakula.
Aina hii huvumilia bungo na ugonjwa wa majani.
Hakika na Wahi: Hizi
ni aina mbili za mtama ambazo zimezalishwa na kituo cha Utafiti wa
Kilimo cha Ilonga kwa ajili ya kuoteshwa kwenye mashamba yalioathiriwa
na viduha. Mbegu hizi zina rangi ya manjano iliyopauka. Unga wa aina
zote mbili zinafaa sana kwa kupika ugali.
Utayarishaji wa shamba na kupanda
Kwa
kawaida mtama hupandwa kwa kutumia mbegu. Mbegu hupandwa shambani moja
kwa moja baada ya shamba kuandaliwa, lakini pia zinaweza kurushwa
shambani, kasha zikavurugwa pamoja na udongo. Unapaswa kutayarisha
shamba la kupanda mtama, iwe ni kwa ajili ya malisho au chakula kabla
mvua za msimu hazijaanza. Zao hili hufanya vizuri zaidi kwenye udongo
ulio laini. Linaweza pia kupandwa kwenye udongo ambao haukulimwa vizuri
na bado ukaota vizuri.
Nafasi: Mtama
unaopandwa kwa ajili ya malisho, unaweza kupandwa kwa nafasi ya
sentimita 75×10. Aina za mtama ambazo zinalengwa kwa ajili ya lishe kwa
binadamu na wanyama, zinahitaji nafasi kiasi cha sentimita 60×20. Nafasi
hutoa mwanya wa kuwa na kiwango kikubwa cha malisho. Mkulima anaweza
kupanda mbegu za mtama kiasi cha kilo 2.4-3.3 kwa hekari moja. Ni mara
chache sana mbegu hupandwa kwenye vitalu na kuhamishiwa shambani
baadaye.
Kupanda: Mtama
hupandwa mvua zinapoanza kunyesha. Mbegu ni lazima zifukiwe ardhini
usawa wa sentimita 3 kwenda chini, hii itasaidia kuepuka kuota wakati
ambao si msimu kamili wa mvua. Pia zinaweza kufukiwa kiasi cha sentimita
2 wakati ardhi inapokuwa na unyevu. Mtama unahitaji rutuba ya hali ya
juu wakati wa kupanda na wakati wa kuota. Ni vizuri kutumia samadi au
mboji iliyooza vizuri wakati wa kuandaa shamba.
Mseto: Unaweza
kupanda mtama mseto na mazao jamii ya mikunde, na kuongeza mboji
shambani mwako. Hii inaweza kuwa njia nzuri zaidi ya kupata virutubisho
vinavyohitajika. Mseto wa mazao jamii ya mikunde inashauriwa iwe ni kama
vile maharagwe, kunde, n.k
Uangalizi na utunzaji
Ni
lazima kung’oa baadhi ya mimea inapokuwa na urefu wa sentimita 30, au
siku 30 baada ya kupanda, ili kuwa na uhakika wa nafasi ya sentimita 10
kati ya mstari na mstari kwa mtama unaokusudiwa kwa ajili ya malisho, na
nafasi ya sentimita 20 kati ya mstari kwa mtama uliokusudiwa kwa ajili
ya chakula na lishe ya mifugo.
Palizi
ya mkono ifanyike walau mara mbili. Shamba la mtama ni lazima liwekwe
katika hali ya usafi na kutokuruhusu magugu wakati wote hasa katika
kipindi cha mwanzoni.
No comments:
Post a Comment